JAJI Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, amewataka watumishi wa Mahakama kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uaminifu na kutochelewesha haki kwa wananchi.
Pia, ameahidi kuchukua hatua kadhaa ili kurahisisha utoaji haki nchini zikiwemo kuimarisha miundombinu ya Mahakama ikiwemo ya majengo na mfumo wa TEHAMA.
Profesa Juma aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa kanda hiyo, alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku nne ya Mahakama, Kanda ya Musoma.
Alisema kuna ulazima mkubwa wa kuhakikisha watendaji wa mahakama wanashughulika na changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi kwa lengo la kuimarisha maslahi yao.
Katika ziara hiyo, Profesa Juma alitembelea Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini, Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na kuwataka watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uaminifu.
Pia, katika ziara hiyo, Jaji Mkuu alipokea taarifa ya utendaji kazi kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini, Prisia Mkeha, inavyofanya kazi kwa kuwahudumia wakazi wa kata 16.
Kata hizo ni Kitaji, Mkendo, Mwigobero, Mwisenge, Makoko, Buhare, Kamunyonge, Nyasho, Nyakato, Mshikamano, Rwamlimi, Bweri, Kwangwa, Kigera, Iringo na Nyamatare.
Prisia alieleza kuwa pamoja na kuhudumia kata hizo, Mahakama yake inakabiliwa na upungufu wa watumishi ambapo mahitaji halisi ni 15, waliopo ni wanane, hivyo kuna upungufu wa watumishi saba wa kada mbalimbali.
Kuhusu hali ya mashauri, Hakimu Mfawidhi alimweza Jaji Mkuu kuwa mashauri yaliyobaki mwaka 2020 yalikuwa 139, wakati 138 yalisikilizwa na kumalizika na kuna shauri moja tu la mwaka huo ambalo lipo katika mlundikano.
Alibainisha pia kuwa mashauri yaliyopokelewa na kusikilizwa kuanzia Januari hadi Septemba, mwaka huu ni 1,048, yaliyosikilizwa 934 na yaliyobaki ni 114.
Kabla ya kutembelea, Mahakama ya Wilaya ya Musoma, Profesa Juma alikutana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Arufani Haule, katika Mahakama ya Mwanzo, ambaye aliupongeza uongozi wa Mahakama kwa juhudi unazofanya katika kuimarisha mfumo wa utoaji wa haki kwa wananchi.
Dk. Haule alimweleza Jaji Mkuu kuwa Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini ndiyo Mahakama pekee inayohudumia Wilaya hiyo, hivyo kwa kuzingatia wingi wa mashauri, idadi ya watu na matukio katika Wilaya, kuna ulazima wa uwepo wa mahakama nyingine.
Katika ziara hiyo, Jaji Mkuu aliambatana na viongozi mbalimbali wa Makao Makuu, wakiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Wilbert Chuma, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Solanus Nyimbi ambaye alimwakilisha Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel, Mtendaji Mahakama Kuu, Masijala Kuu, Samson Mashalla, ambaye alimwakilisha Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Leonard Magacha’
Na FAUSTINE KAPAMA, Mahakama-Musoma