MSAJILI wa Vyama vya Siasa Nchini Jaji Francis Mutungi, amesema ameandaa kikao kazi cha majadiliano kati yake, polisi na viongozi wakuu wa vyama vyote vilivyokamilisha usajili, kutafuta suluhu ya masuala muhimu kwa mustakabali wa siasa za Tanzania.
Ameitaja ajenda kuu ya kikao hicho kuwa ni kutafuta muarobaini wa hali inayoonekana kama mivutano baina ya Jeshi la Polisi Nchini na vyama vya siasa katika harakati zao za kufanya siasa, hususan mikutano na makongamano.
Jaji Mutungi ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi huo wa ofisi yake ili kumaliza hali hiyo ambayo amesema imeachwa mpaka imejenga taswira hasi kwa umma.
“Yawezekana umma ukafikiri kwamba tumekalia kimya hili suala na hakuna namna yoyote umma watajua kinachofanyika, hivyo nikaona ni busara tuwaite (waandishi wa habari), tuuhabarishe umma kwamba hatujakalia kimya hii hali ambayo naamini ni kama inaleta taharuki fulani.
“Msajili ni kama mlezi wa vyama vya siasa na msimamizi wa sheria ya vyama vya siasa, niliwasiliana na IGP na tutakubaliana kimsingi tuwaite wadau… Tunaposema wadau ninamaanisha vyama vya siasa, kwenye suala hili,” amesema Jaji Mutungi.
Jaji Mutungi amesema, wakati maandalizi ya kikao hicho yakiendelea, ofisi yake inavitaka vyama vya siasa na viongozi wao kuwa watulivu, kusubiri kukamilika kwa maandalizi hayo na kufanyika kwa kikao husika ambacho kitatumika kujibu maswali yao mengi.
Amesema utulivu huo, unahusisha pia kutofanyika kwa makongamano na mikutano ya kisiasa ambayo kutokana na hali iliyopo, upo uwezekano wa watu kujenga hofu kila wanaposikia wito wa mikutano ya kisiasa kutokana na ushiriki wa idadi kubwa ya polisi katika mikutano hiyo.
“Tusingependa pia ifike mahala watu waanze kuogopa kila mkutano wa siasa mapolisi wamejaa, kila shughuli ya wanasiasa, mapolisi wamejaa… tumeliona hilo na tunawaita wadau tuelimishane na tukitoka hapo wadau wenyewe ndo watarudi kwa umma kueleza picha halisi,” amesema.
Msajili huyo amesema, katika udadisi uiofanywa mitandaoni ambako majibizano mbalimbali ya kisiasa yanafanyika, ofisi ya msajili imebaini kuwa wapo baadhi ya watu au kundi linahitaji kuelezwa zaidi juu ya sheria zinazosimamia masuala ya mikutano ya kisiasa.
“Tunataka kuondoa ile hali inayoonekana kuwa wanasiasa wanakosea hapa, vyama vya siasa navyo vinakosea hapa, tukaona kwanini tusikae meza moja na kuzungumza na kuweka bayana wapi tumepishana, hakuna mahali tunataka kusemana taasisi fulani inavunja katiba, ni katika kueleweshana tu,”
Amesisitiza kuwa, siasa za Tanzania hazijafikia hatua ya kuwepo kwa taharuki na sintofahamu ambayo imekosa suluhu, huku pia akieleza kuwa mbali na mazungumzo hayo yanayotarajiwa, vyama vya siasa vina fursa nyingine ya kuzungumza na Rais Samia Suluhu Hassan, wakati muafaka utakapowadia.
Kadhalika amesema umma unatakiwa kuendelea kuwaamini wanasiasa na vyombo vya ulinzi vinavyosimamia amani, kwa sababu vina uchungu na uzalendo wa nchi hii tofauti na inavyodhaniwa na baadhi ya watu, walioyaweka makundi haya kwenye mtazamo hasi.
MREJESHO UHAKIKI WA VYAMA
Akizungumza pembeni ya mkutano huo wa wanahabari, Msaidizi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, amesema uhakiki unaendelea kulingana na ratiba iliyotolewa awali, lakini changamoto kubwa iliyobainika kwa kiasi kikubwa hadi sasa ni ukosefu wa weledi katika utunzaji wa taarifa za mapato na matumizi ya vyama vya siasa nchini.
Sisty amesema kutokana na changamoto hiyo, wametoa muda zaidi kwa vyama vyote vilivyokutwa na dosari hiyo, ili kuandaa taarifa rasmi ambayo itatakiwa kuwasilishwa kwa ofisi ya msajili ndani ya muda uliotolewa.
Agosti 29, mwaka huu, Nyahoza kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, alieleza kuwa Msajili ameviita vyama 19 vya siasa vyenye usajili kamili kwa upande wa Tanzania Bara na visiwani, katika uhakiki ulioanza Agosti 30, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uhakiki huo unafanyika katika ofisi za vyama vya siasa zilizopo Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar hadi Septemba 24, mwaka huu hatua ambayo ni takwa la kisheria, katika kuhakikisha vyama 19 vyenye usajili kamili, vinatekeleza masharti ya usajili kama yalivyoainishwa kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa na kanuni zake.
Pia alifafanua katika taarifa hiyo kuwa, sababu ya uhakiki huo kufanyika Bara na visiwani, ni kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, inayoelekeza kila chama chenye usajili kamili kuwa na ofisi pande zote mbili za Muungano.
Na WILLIAM SHECHAMBO NA SAMIRA OMARY (TUDARco)