RAIS Samia Suluhu Hassan, amemteua Jaji Jacob Mwambegele kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Jaffar Haniu, ilisema Jaji Mwambegele ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mjumbe wa NEC.
Ilisema Jaji Mwambegele anachukua nafasi ya Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Semistocles Kaijage ambaye amemaliza muda wake.
Wengine walioteuliwa na Rais Samia ni Jaji Mwanaisha Kwariko aliyeteuliwa kuwa Mjumbe wa NEC, ambaye anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Mwambegele.
Pia, Rais Samia amewateua Jaji Sam Rumanyika, Jaji wa Mahakama Kuu kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani na Profesa Khamis Dihenga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Taarifa hiyo ilisema kabla ya uteuzi huo, Profesa Dihenga anahudumu kwa mkataba katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Morogoro.
Ilisema Profesa Dihenga anachukua nafasi ya Profesa William Anangisye aliyemaliza muda wake na amemteua Dk.Mussa Kissaka ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).
Taarifa hiyo ilisema uteuzi huo ulianza Desemba 23, mwaka huu.
Na Mwandishi Wetu