VIONGOZI wapya wa Chama cha wafanyakazi wa sekta za utafiti, taaluma na mashirika (RAAWU), Mwenyekiti Jane Mihanji na Katibu Mkuu, Joseph Sayo, wamesema kwasasa wataongoza chama hicho kwa misingi na kanuni zilizowekwa na wanachama wote ikiwemo ya umoja na mshikamano.
Jane Mihanji ambaye pia ni Kaimu msanifu Mkuu wa Kurasa wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo yanayochapwa na kampuni ya UMGL, alishinda nafasi hiyo kwa kura 42 dhidi ya mpinzani wake Laison Mwalembe aliyepata kura 35, katika nafasi ya Katibu Mkuu, Sayo alishinda kwa kura 41 huku mpinzani wake Simon Mbai akipata kura 34.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi mwishoni mwa wiki iliyopita, Jane alisema silaha namba moja ya maendeleo ya Raawu ni umoja na mshikamano wa wanachama.
Jane alisema anaamini kupitia umoja na mshikamano wa wanachama RAAWU itafika mbali, kwani matabaka ni adui wa mafanikio.
“Nafurahi kwa ushindi huu, lakini nawaomba sana wanachama wenzangu tuwe na umoja na mshikamano, tusahau matabaka tuliyokuwa nayo zamani, kupitia silaha ya umoja na mshikamano, Raawu itakuwa imezaliwa upya na yenye mafanikio,” alisema Jane Mihanji.
Naye Katibu Mkuu Sayo alisema kupitia uchaguzi huo, anaamini utakuwa ni mwanzo mwingine na bora kwa chama hicho na anaahidi kushirikiana vyema na wanachama kuhakikisha wanakikuza chama.
Kwa mujibu wa muhtasari wa ripoti ya mkutano wa sita wa chama hicho, Raawu ina zaidi ya wanachama 9000 kutoka nchi nzima.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Ijumaa na kumalizika asubuhi ya Jumamosi iliyopita, nafasi nyingi ziligombewa ikiwemo Naibu Katibu Mkuu, Wawakilishi Mkutano Mkuu TUCTA, nafasi za wanawake, vijana, wajumbe wa Baraza Raawu na TUCTA pamoja na Wajumbe Kamati ya Utendaji Raawu (KUT).
Na Abdul Dunia