WAZIRI wa Nishati, January Makamba, ameanza kutembelea mito inayoingiza maji katika mabwawa ya vituo vyote vya kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji.
Katika ziara hiyo, January aliambata na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Maharage Chande na maofisa wengine wa shirika hilo.
Aidha, January alielekeza TANESCO kutokodi mitambo ya dharura kutokana na historia mbaya ya mitambo ya aina hiyo kuwa na gharama kubwa kwa serikali na kughubikwa na utata.
Ziara hiyo ililenga kutathmini hali halisi ya ukame katika mito hiyo, kiwango cha maji katika mabwawa, uzalishaji katika vituo na kutathmini hatua za kuchukua kukabiliana na changamoto hiyo.
January alishuhudia mtiririko hafifu katika Mto Ruaha na kukauka kwa mito midogo inayochangia katika mtiririko wa Mto Ruaha na bwawa dogo la Kidatu.
Hali hiyo imesababishwa na ukame unaotokana na kutonyesha mvua katika maeneo yanayolisha mito hiyo, matumizi mabaya ya rasilimali maji na uharibifu wa mazingira katika maeneo husika.
Hali hiyo ya ukame imesababisha upungufu wa megawati 307 kati ya megawati 561 zinazopaswa kuzalishwa kutokana na nguvu ya maji.
Akizungumza na wafanyakazi wa TANESCO na viongozi katika maeneo husika, Waziri huyo alisema ni dhahiri kuna ukame ambao umeathiri mtiririko wa maji, hivyo kuathiri uzalishaji wa umeme.
Alielekeza shirika kuhakikisha linaongeza miradi mipya ya uzalishaji umeme kwa njia ya upepo na jua ambayo inaweza kutekelezwa ndani ya mwaka mmoja ili mwakani katika kipindi kama hiki taifa lisikabiliwe na uhaba wa umeme.
Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Chande alisema shirika linachukua hatua za haraka kuongeza uzalishaji kwa kutumia gesi asilia, kuharakisha matengezo ya baadhi ya mitambo ya Ubungo I (MW 25) upanuzi wa Kinyerezi I (MW 185) na Ubungo III (MW 112).
Alisema shirika limelazimika kuwasha kituo cha kuzalisha umeme cha Nyakato (MW 36).
Chande alisema hatua zitakazokamilika kwa hatua kuanzia Desemba 2021 hadi Machi, mwakani zitasaidia kuongeza MW 350 katika mfumo wa gridi ya taifa.
Pia, shirika linaendelea na matengenezo na maboresho ya mfumo wa usambazaji na ugavi wa umeme ikiwemo kuharakisha maboresho ya miundombinu ya kusafrisha umeme ya 220 kV Kidatu – Iringa, 220kV Kingolwira – Msamvu na vituo vya kusambaza umeme vya Msamvu, Luguruni, Kunduchi na Nyakanazi.
Chande alifafanua zaidi kuwa TANESCO itafanya maboresho katika njia za kasambaza umeme ambazo kwa sasa ni ndefu na zinapelekea wateja kupata umeme hafifu na uharibifu wa mara kwa mara wa mita.
Na Mwandishi Wetu