MAHAKAMA Maalumu ya kesi za udhalilishaji wa kijinsia iliyopo Vuga, Mkoa wa Mjini Magharibi, imemhukumu Shaibu Hussein Shehe kutumikia kifungo cha miaka 37 jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa matatu likiwamo la kumtorosha mtoto mwenye miaka 15.
Kesi ya Shaibu (30), iliripotiwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Vuga mnamo Septemba 18, 2019 na kuanza kutajwa Januari 14, 2020.
Mshitakiwa huyo, alitiwa hatiani kwa makosa ya kubaka, kulawiti na kutorosha mtoto ambaye yupo chini ya uangalizi wa wazazi wake.
Mwendesha mashtaka wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Hariri Ishau, alidai mtuhumiwa alimtorosha mtoto huyo na kwenda nyumbani kwao Mwanyanya kisha vitendo vya udhalilishaji.
Jumla ya mashahidi sita, walitoa ushahidi wao mbele ya Hakimu Makame Mshamba ambaye aliridhishwa na pande zote mbili, ndipo alipoamua kumtia hatiani mtuhumiwa kwa kutumikia Chuo cha Mafunzo miaka 37.
Mshamba alidai mtuhumiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 kwa kosa la kubaka na kumuingilia kinyume cha maumbile, mtuhumiwa atatumikia miaka saba, adhabu zote hizo zitakwenda pamoja.
“Mahakama ya Vuga imemtia hatiani mtuhumiwa Shaibu Hussein Shehe kwenda jela miaka 37 kwa makosa matatu ya udhalilishaji wa kijinsia, pia atalazimika kutoa fidia ya sh. 500,000,”alisema.
Hiyo ni adhabu ya kwanza kwa mahakama ya udhalilishaji wa makosa ya ubakaji kwa mwaka huu.
NA WAANDISHI WETU, ZANZIBAR