MKUU wa Majeshi ya Ulinzi Nchini, Jenerali Venance Mabeyo, amewasamehe vijana 853 kati ya 854 waliofanya vitendo vya kukiuka nidhamu jeshini na kuamuru kuwa, wote warejeshwe katika makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), tayari kwa kuendelea na mafunzo yao.
Ameagiza kuwa, vijana hao wapokelewe katika Kambi ya Kujenga Taifa Kikosi Namba 841, iliyopo Mafinga mkoani Iringa Machi 12, mwaka huu huku utaratibu mwingine utaelekezwa baada ya kupokelewa.
Hata hivyo, mmoja kati ya vijana hao 854 amefariki na idadi yao kubaki 853.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya zamani ya Jeshi, Upanga Ngome jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano na Msemaji Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Kanali Gaudentius Ilonda, alisema Jenerali Mabeyo alitoa msamaha huo baada ya uchunguzi na utafiti uliofanywa kwa kina na kubaini sababu ambazo zilifanywa na vijana hao.
Alizitaja sababu hizo kuwa ni vijana wengi walifanya vile kutokana na utoto wao na kutojitambua, huku wengine walifanya kwa kurubuniwa na wengine walifanya kwa kufuata mkumbo.
“JWTZ imefanya uchunguzi kwa vijana hao, kila mmoja mahali alipo walipokatishwa mafunzo hadi kufikia sasa, Jeshi limekwenda mkoa kwa mkoa, wilaya kwa wilaya, Tarafa kwa Tarafa na Kata kwa Kata hadi vijijini na kujiridhisha kwamba, vijana hao wamechunguzwa hadi kwa ngazi ya familia bila familia na vijana wenyewe kujua nini kinaendelea,” alisema.
Alisema baada ya uchunguzi huo, JWTZ imejiridhisha pasipo na shaka kwamba, vijana hao kwa sasa mwenendo wao ni wa kuridhisha na wanastahili msahama waliopatiwa, hivyo ameomba umma wa Watanzania kuendelea kuwaamini.
“Tuwe tayari kuwapa nafasi nyingine waendelee na mafunzo yao,” alisema.
Aidha, JWTZ ilisisitiza kuwa, vijana wanaohusika kurudi kambini ni wale walioachishwa mafunzo na kufukuzwa kutokana na sababu za makosa ya nidhamu na kurejeshwa makwao mwaka jana.
Hivyo, jeshi hilo, liliwataka wale wote wasiohusika na msamaha huo kutojaribu kudanganya kwa kuwa, Jeshi limeenda mbali zaidi kwa kujua kwamba, katika msafara wa mamba na kenge watajipenyeza.
Kutokana na hali hiyo, aliwatahadharisha vijana ambao hawahusiki na msahama huo, kutofanya udanganyifu kwa sababu orodha yote imeandaliwa na picha zao pamoja na makundi yao ya damu.
Pia, aliuomba umma wa Watanzania kuacha vitendo vya kuwarubuni vijana hao hasa wanapokuwa kambini katika kambi za kujenga Taifa, wawaache wapatiwe mafunzo ya stadi za maisha ili waje kulitumikia Taifa lao kwa moyo mmoja.
UAMUZI
Mapema mwaka jana Aprili 17, Jenerali Mabeyo, aliwafukuza vijana 854 wa JKT waliokiuka taratibu kwa kuanzisha mgomo na kuandamana kwenda Ikulu wakishinikiza kuajiriwa jeshini.
“Aprili 8, 2021 vijana wetu wa JKT wapatao 854, walianzisha mgomo, kukataa kufanya kazi maeneo mengine na kufanya maandamano kwenda Ikulu, kwa madai ya kutaka kumuona Rais ili wadai kuandikishwa jeshini kama walivyoahidiwa na aliyekuwa Rais Hayati John Magufuli.”
Aprili 16, mwaka jana, katika hafla ya kuwatunuku kamisheni maofisa wa JWTZ mjini Dodoma, Jenerali Mabeyo alisitisha mikataba yao na kuwaamuru warudi nyumbani.
Na Jacqueline Massano