JESHI la Kujenga Taifa (JKT) linatekeleza kwa vitendo agizo la Serikali la kulima mazao ya kibiashara na ya kimkakati ambapo wanalima ekari 107, ekari 7 ndani yake ni kwa ajili ya kitalu cha mbegu la zao la mkonge katika Kikosi cha Mgambo 835 Kj, kilichopo mkoani Tanga lengo likiwa ni kulima ekari 200.
Mapema mwanzoni mwa mwaka huu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua zoezi la ugawaji wa miche bora ya Mkonge iliyozalishwa na kituo cha utafiti wa zao la Mkonge wilayani Muheza aliagiza uzalishaji wa mbegu hizo kufanyika katika kila halmashauri inayozalisha mkonge katika mkoa wa Tanga.
Mkurugenzi wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Kanali Peter Lushika, akizungumza na waandishi wa habari waliofanya ziara maalum ya kukagua shamba la mkongo na kujionea shughuli za kilimo mkakati zinazotekelezwa katika Kikosi hicho, amesema huo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika hotuba yake.
Kanali Lushika amesema zao la mkonge katika Kikosi hicho cha Mgambo ni zao jipya ambalo ni la kibiashara licha ya kuwa katika Kikosi hicho pia wanalima Michungwa na Mahindi.
“Sisi JKT tumekuwa wakwanz kuitikia wito wa serikali kila unapotolewa, hivi sasa tunatekeleza kwa vitendo mazao ya kilimo mkakati ambayo yanalimwa kibiashara ikiwemo zao la Mkonge ambalo tunalilima katika Kikosi hiki Cha Mgambo,”amesisitiza.
Amesema mbali na kilimo hicho cha kimkakati pia wanazalisha mbegu za mkonge kwa alisilimia 100 na mbegu za mazao mengine lengo likiwa ni kuhakikisha hawaagizi mbegu kutoka nje ya nchi.
Mkurugenzi huyo ambaye pia ni Katibu wa Kilimo, mkakati Mifugo na uvuvi amefafanua kuwa JKT inahakikisha nchi inakuwa na usalama mkubwa wa chakula na kwamba mkakati wa JKT ni kuhakikisha wanazalisha mbegu bora.
Meja Lushika alisema wanakusudia kila zao linalozalishwa na JKT linaenda kuchakatwa na Viwanda vya Jeshi hilo ikiwa ni sehemu ya jeshi hilo kujitegemea pia wanazalisha mazao na mbegu Bora kwa mazao yote ya kimkakati ikiwemo Kahawa, Mkonge na Korosho.
Pia ameeleza kuwa JKT imekuwa ikitekeleza agizo la Serikali kwa vitendo hivyo imekuwa ikilima mazao ya mkakati Kama vile Mkonge, Kahawa, Korosho na Mchikichi.
Awali Kaimu Kamanda Kikosi hicho Meja Raymond Mwanri, amesema walianza kutekeleza agizo la Serikali kwa kulima ekari 100 za Mkonge Juni mwaka huu kwa kuandaa shamba.
Naye kijana wa kujitolea katika kikosi hicho Hamad Shame amesema anaishukuru Serikali kwa kuwapa fursa hiyo ya kuja kujifunza kwa vitendo katika Kambi hiyo.
Na Happiness Mtweve,Dodoma