SERIKALI imesema Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lipo tayari na limejipanga kupambana dhidi ya matukio ya kigaidi kabla hayajatokea na kuleta madhara.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax, wakati akieleza mafanikio ya wizara hiyo yaliyopatikana katika miaka 60 ya uhuru.
“Niwahakikishie, muwe na amani, jeshi letu lipo limejipanga kuhakikisha yanapotokea mashambulio kama hayo ya kigaidi, yanadhibitiwa kabla hayajatokea.
“Na hata yakitokea tayari tumejipamga vile vile, suala hili si la kwetu bali ni la kidunia na ndio maana tunafanya kwa kushirikiana na wenzetu,” alisema waziri huyo.
Aliongeza kuwa: “Kama mnavyofahamu hivi sasa baadhi ya askari wetu wapo Msumbiji na kilichowapeleka kule ni kupambana dhidi ya ugaidi, tunaamini wakiwa huko watabadilishana mawazo namna ya kukabiliana na kuendeleza ushirikiano baina yetu.”
ULINZI WA MIPAKA
Waziri huyo alisema serikali kupitia JWTZ imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda mipaka ya nchi na kuhakikisha inakuwa salama.
Alisema mipaka hiyo inajumuisha eneo la nchi kavu, anga na eneo la maji ambapo kwa kipindi kirefu imeendelea kuwa salama.
“JWTZ imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa hali ambayo imesaidia nchi kuwa salama katika anga, maji, nchi kavu na mipaka kwa ujumla,” alisema.
USHIRIKI WA JWTZ KULINDA AMANI
Kuhusu ulinzi wa amani, waziri huyo alisema JWTZ imeendelea kushirikiana na mataifa ya Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) katika operesheni ya ulinzi wa amani.
Alibainisha kuwa ushirikiano huo ulihusisha kupeleka majeshi katika nchi ambazo zimekuwa na migogoro, vikosi, waangalizi wa kijeshi, wanadhimu na makamanda.
Alizitaja nchi ambazo JWTZ imewahi kushiriki katika ulinzi wa amani kuwa Liberia, Eritrea, Shelisheli, Ivory Coast, Sierra Leon na Sudan.
Alisema kwa sasa JWTZ inashiriki ulinzi wa amani katika nchi za Lebanon, Jamhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC), Jamhuri ya Afrika ya Kati, Msumbiji na Sudan Kusini.
MAFUNZO YA JKT
Dk. Stergomena alisema tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), limeendelea kutekeleza mafunzo kwa vijana kwa ufanisi hadi mwaka 1994 yalipositishwa.
“Hatua ya kufuta JKT ilichukuliwa na serikali kutokana na kuyumba kwa uchumi wa dunia mwaka 1980 hadi 1990, hivyo serikali ililazimika kusitisha mafunzo hayo kwa muda,” alieleza.
Waziri huyo alieleza kuwa mafunzo hayo yalirejeshwa mwaka 2001 kwa vijana wa kujitolea na mwaka 2013 kwa mujibu wa sheria ambapo hadi sasa yameleta mafanikio makubwa.
Alitaja mafanikio hayo ni kuongezeka kwa uzalendo kwa vijana na kupunguza migomo ya vyuo vikuu na maeneo ya kazi.
MAFUNZO YA KIJESHI
Dk. Stergomena alisema JWTZ imeendelea kutoa mafunzo ya kozi za kijeshi katika shule na vyuo vya kijeshi ndani na nje ya nchi.
Alifafanua kwamba lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kiutendaji kivita maofisa na askari katika kutekeleza majukumu yao ya msingi ndani na nje ya nchi.
Aliongeza kuwa kwa kutambua hilo serikali kupitia wizara yake imeendelea kuimarisha shule na vyuo vya kijeshi ikiwa ni jitihada za kuboresha mafunzo.
“Baadhi ya vyuo na shule ni Chuo Cha Taifa cha Ulinzi (NDC) Chuo cha Ukamanda na Unadhimu (CSC-Duluti), Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) na Shule ya Awali ya Kijeshi-RTS Kihangaiko,” alizitaja.
KILIMO CHA KIMKAKATI
Waziri huyo alibainisha kwa JKT imeendelea kutekeleza mkakati wa kilimo 2019 hadi 2025 wa kuliwezesha jeshi hilo kujitosheleza kwa chakula.
Alisema mkakati huo umetekelezwa kwa vitendo katika vikosi vya Chita mkoani Morogoro, Milundikwa Rukwa, Mlale Ruvuma, Tanga na Oljoro Arusha kwa kutumia vyanzo vya ndani vya mapato vya JKT na serikali.
“JKT inaendelea kushiriki katika kilimo cha mazao ya kimkakati ya taifa ambayo ni Michikichi, Nachingwea na Manyoni Singida, alizeti Makutupora Dodoma na Kahawa Itende mkoani Mbeya na Tarime mkoani Mara.
Aliongeza kuwa: “katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi wizara kupitia JKT inaendelea na ujenzi wa mfumo wa umwagiliaji katika shamba la mpunga Chita.”
NA FRED ALFRED, DODOMA