WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Doroth Gwajima, amesema katika kukabiliana na ongezeko la watoto wa mitaani, Serikali imeunda kamati mbalimbali ili kushughulikia watoto hao wasiweze kuongezeka.
Akaonya kuwa wazazi waache kuwatumikisha watoto kwa kuwatuma kuomba mitaani.
Pia, amesema katika Mkoa wa Dar es Salaam pekee, Serikali imetambua watoto 5,390 kati yao, wavulana ni 3,452 na wasichana 1,538 ambao tayari wamepewa huduma mbalimbali ikiwemo vifaa vya shule na huduma mbambali za kuimrisha pato la kaya zao.
Akizungumza juzi usiku Jijini Dar es Salaam wakati wa chakula cha pamoja na watoto wa mitaani iliyofanyika Ukumbi wa Karimjee, Dk. Gwajima, alisema watoto 135 wameunganishwa na familia zao, wasichana walikuwa 43 na wasichana 92.
“Kuna tatizo la watoto wanaoshi mitaani hasa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Iringa na Dodoma.
“Kati ya watoto 5,390 tuliowatambua, 3,452 walikuwa wavulana na 1,538 walikuwa wasichana, hawa walitambuliwa na kupewa huduma mbalimbali, wengine 135 waliunganishwa na familia, wavulana walikuwa 92 na wasichana 43,”alisema
Akifafanua kuhusu watoto waliopata huduma mbalimbali, Dk. Gwajima alisema watoto 821 walipewa vifaa vya shule na wengine 75, walipewa huduma ya kuimarisha pato la kaya.
“Kuna hizi kamati ambazo zimeandaliwa na Serikali inaitwa MTAKUA, huu ni Mpango Kazi wa kutokomeza ukatili kwa watoto na wanawake, unaisha Juni, lakini kuna mwingine utaanza, watoto wanazidi kuongezeka lazima sasa twende katika suluhu ya kuwaondoa mtaani na kuzuia wengine wasije,” alisema
Dk. Gwajima alieleza kuwa, Serikali itaendelea kupitia sera na sheria zilizopitwa na wakati kisha kuzirekebisha kwani haikuwa tayari kuendelea kushuhudua watoto wakihangaika mitaani ikiwemo kulala chini ya madaraja.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala alisema kwamba, amewaagiza Wakurugenzi kufanya sensa ya Watoto hao ili kujua ukubwa wa tatizo kimkoa.
Na IRENE MWASOMOLA