MAHAKAMA ya Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu, imemhukumu karani wa Baraza la Ardhi na Nyumba, wilayani humo, Tito Kabume, kutumikia kifungo cha miaka 10 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia sh. 480,000 kwa njia ya udanganyifu.
Inadaiwa mshitakiwa huyo alijipatia fedha hizo kwa nyakati tofauti kupitia kwa njia ya mtandao.
Hukumu hiyo ilisomwa mwishoni mwa wiki na Hakimu Mkazi, Enos Misana, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa Jamhuri.
Hakimu Misana alisema mshitakiwa alikuwa anakabiliwa na mashitaka mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu akiwa mtumishi wa serikali.
Alisema katika shtaka la kwanza, mshitakiwa huyo alikuwa akidaiwa kujipatia sh 180,000 kwa njia ya udanganyifu na la pili kujipatia sh. 300,000 kwa njia ya udanganyifu kupitia mtandao wa simu ya mkononi.
Akitoa adhabu, Hakimu alisema mshitakiwa huyo atatumikia kifungo cha miaka mitano jela kwa kila kosa.
Awali, Wakili wa Serikali, Rehema Sakafu, alidai mshitakiwa akiwa mtumishi wa baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Maswa, Agosti 17, mwaka 2019 alipokea sh. 140,000 na Agosti 31, 2019 alipokea sh. 40,000 kutoka kwa Lazaro Butegi.
Wakili huyo alidai mshitakiwa huyo alipewa fedha hizo ili ampelekee Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jackson Kinyeriyeri, kwa lengo la kutoa upendeleo katika shauri la rufani la ardhi namba 53/2018, wakati hakutumwa kufanya hivyo na mwenyekiti huyo.
Pia, mshitakiwa huyo alikuwa akidaiwa kwamba Julai 26, 2019 alipokea sh. 150,000 na kiasi kama hicho tena kutoka kwa Ibrahim Kitama ili ampatie upendeleo katika shauri dogo la ardhi Na.139/2016 huku akidanganya fedha hizo zimeombwa na mwenyekiti wa baraza hilo, Kinyerinyeri, wakati akijua si kweli.
Baada ya mshitakiwa kutiwa hatiani, Wakili wa Serikali wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Albertina Mwigilwa aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwake na wengine.
Na Costantine Mathias,Maswa