RAIS wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) kwa kufanya kazi nzuri na kuwarahisishia wafanyabiashara wa nchi hiyo, katika suala zima la usafiri.
Pia, ameishukuru TPA kwa kufungua ofisi zao nchini Burundi, jambo linalowasaidia wafanyabiashara wa nchi hiyo kufanya biashara zao kwa urahisi hususan katika usafirishaji wa bidhaa na mizigo.
Aliyasema hayo, alipofanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam.
“Msichoke kuwahudumia wafanyabiashara wa Burundi. Hapa mlipofika ni pazuri na mmerahisisha biashara za Burundi kwenda vizuri,” alisema Rais huyo na kuongeza kuwa;
“Naishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kurahisisha usafiri wa Burundi, ambapo hivi sasa imeanza kujenga reli ambayo itafika hadi Burundi,” alisema.
Rais huyo alimshukuru Rais Samia kwa mapokezi makubwa aliyompatia yeye na msafara wake na kuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki Tanzania.
TPA YAFUNGUA
Akitoa salamu zake za shukrani kwa Rais wa Burundi, Mwenyekiti wa Bodi ya TPA, Ignas Rubaratuka, alisema ziara hiyo ni uthibitisho kuwa nchi hizo zina zina uhusiano mkubwa wa kibiashara.
“Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, itatekeleza maazimio yote yanayohusu shughuli za uchukuzi kwa upande wa bandari.
“Itatoa kipaumbele kuhudumia shehena za Burundi na kuhudumia zile za wafanyabiashara hao ili waifanye Bandari ya Dar es Salaam kuwa ni chaguo lao la kwanza kwa kusafirisha mizigo yao,” alisema.
MAFANIKIO YA BANDARI
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Erick Hamis, alisema Bandari ya Dar es Salaam ni ya tatu katika nchi za Afrika katika utoaji wa huduma bora na wamekuwa na mafanikio makubwa.
Alibainisha hali hiyo imetokana na uboreshaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika Bandari ya Dar es Salaam kuanzia gati namba 0 hadi namba saba ili kuhakikisha uwepo wa ubora katika ufanyaji wa biashara.
Kwa mujibu wa Erick, bandari hiyo ina jumla ya gati 12, zote zina urefu wa mita 2,482 na zina uwezo wa kupaki meli 11 zenye urefu wa mita 200 hadi 260 na kuhudumia shehena za magari.
“Jana bandari yetu ilihudumia meli 20. Idadi hiyo huwezi kuipata katika bandari nyingine katika nchi za Afrika kutokana na ubora wa bandari ndani ya nchi zote za Afrika,“ alisema.
Alisema japokuwa dunia imekuwa na ugonjwa wa corona, lakini bado bandari imekuwa na ufanisi mkubwa wa kupokea meli nyingi na kubwa na kuonyesha umuhimu wake ndani ya Afrika.
“Bandari yenye meli nyingi ni meli tisa hivyo, inaonyesha kuwa, Tanzania tunaendelea kufanya vizuri katika utendaji wa bandari,”alisema.
Alisema serikali ya awamu ya sita, imeamua kuboresha bandari ya Dar es Salaam ambapo hivi sasa, wanaongeza kina cha lango la kuingilia bandarini na eneo la kugeuzia meli.
Pia, alieleza wameamua kuboresha uhusiano mzuri na nchi ya Burundi katika suala nzima la biashara, ndiyo maana wamefungua ofisi nchini humo, kwa lengo la kuendeleza ufanisi wa bandari.
“TPA itaendelea kuipatia Burundi huduma bora na nchi zingine ambazo zinategemea bandari ya Dar es Salaam katika suala zima la usafiri,” alisema.
WAZIRI AANIKA MABORESHO
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alibainisha kuwa, Bandari ya Dar es Salaam ndiyo kubwa nchini, ni lango kubwa la uchumi wa nchi na hata kwa nchi za jirani kwa kuwa mizigo mingi hupita katika bandari hiyo.
Alisema serikali baada ya kuona hilo, imefanya upanuzi mkubwa katika bandari hiyo kuanzia gati 0 hadi namba saba kwa kufanya uboreshaji mkubwa uliotumia sh. trilioni moja.
Profesa Mbarawa, alifafanua kuwa, lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha meli kubwa na zenye kina kirefu na urefu mkubwa, zinaingia na kwamba, inaendelea kuboresha lango la kuingia na kugeuzia meli, mradi huo utagharimu sh. bilioni 291 na kazi hiyo imeanza, itamalizika baada ya miezi 16.
“Tunategemea mabadiliko chanya katika bandari hii baada ya maboresho hayo ambayo mengine hivi sasa yameshaanza kuonekana,“ alisema.
Aliongeza kuwa, katika robo ya kwanza ya mwaka 2021/2022, magari yaliyohudumiwa katika bandari hiyo, yaliongezeka kutoka 33,481 hadi 455,053 sawa na asilimia 36.
Profesa Mbarawa, alieleza mizigo imeongezeka kutoka tani milioni 4.28 hadi tani milioni 4.93 sawa na ongezeko la asilimia 15, ukilinganisha na mwaka 2021 huku meli zilizoingia katika bandari hiyo, zikiongezeka kutoka 1,053 hadi 1,163 sawa na ongezeko la asilimia 10.
Aidha, alisema makasha (makontena) yaliongezeka kutoka 185,857 hadi 195,320 kwa robo mwaka ya mwaka huu ambayo ni ongezeko la asilimia tano na kwa upande wa mizigo ya Burundi inayohudumiwa katika bandari hiyo kwa mwaka 2020/2021 ni tani 513,544 zilizohudumiwa.
Hata hivyo, alisema Wizara yake, inawashukuru watu wote wanaotumia bandari hiyo, eneo hilo litaendelea kutoa huduma bora kwa saa 24.
RAIS SAMIA, NDAYISHIMIYE WAAGANA
Baada ya kumaliza ziara bandarini, Rais Ndayishimiye alikwenda uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, ambapo aliagana na Rais Samia, akihitimisha ziara ya kikazi ya siku tatu.
Katika ziara hiyo, Rais Ndayishimiye alitembelea Zanzibar maeneo ya historia ya Kanisa Kuu la Anglikana lililopo mji mkongwe eneo la Fumba na kukutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyempongeza Ndayishimiye kwa kuiongoza vizuri Burundi na kurudisha amani na utulivu.
Na REHEMA MAIGALA