KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kenani Kihongosi, amesema Chama hicho, hakitofumbia macho ubadhilifu wa fedha za umma na uzembe kwa watendaji wa serikali.
Hata hivyo, ameagiza kufanywa uchunguzi katika mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mtwara Vijijini, ambayo taarifa zinaonyesha kuna ukiukwaji wa taratibu za manunuzi.
Akizungumza katika ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Mtwara vijijini Katibu Mkuu, alisisitiza wajibu wa CCM ni kuisimamia serikali iliyoiunda na kufikisha maendeleo kwa wananchi kwa wakati ili wapate huduma bora katika maeneo yao.
Alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kufanya mpinduzi ya kiuchumi katika sekta mbalimbali na kuhakikisha inafikisha maendeleo kwa wananchi wa chini.
“Mimi ni kijana aliyeniamini katika kutumikia taifa letu nipo tayari kuwasaidia wananchi wa Mtwara vijijini kuhakikisha kwa wakati na huduma zinawafikia kwa wakati ili muendelee kumuunga mkono rais wetu,” alisema.
Alibainisha kuwa watakuwa wakali katika kuisimamia serikali kwani ni wajibu wa CCM kufanya hivyo, ili kuhakikisha Ilani inatekelezwa kama ilivyoahidiwa.
Mbali na hayo Katibu Mkuu huyo, alieleza kufuirahishwa na mradi wa tofali unaotekelezwa na vijana kutokana na fedha za mkopo usio na riba kutoka katika Halmashauri hiyo na kuzitaka nyingine kuhakikisha zinatenga fedha hizo na kuzifikisha kwa walengwa.
Aliagiza kutunzwa kwa miundombinu ya shule ya Dinyecha iliyojengwa kwa ubora na thamani ya fedha inaonekana, akisema kufanya hivyo ni kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Aliwasihi wananchi wa Mtwara kuendelea kuwa na imani na CCM, pia kumuunga mkono Rais Samia ambaye amekuwa mstari wa mbele kutekeleza Ilani ya Chama.