MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, imeshindwa kuanza kusikiliza kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuwasilisha mashahidi.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Salome Mshasha, Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili Trasila Asenga, huku Sabaya na wenzake wakiwakilishwa na Dankan Owora na Mosses Mahuna.
Kesi hiyo ya jinai namba 27 ya mwaka huu, ilipangwa kuanza kusikilizwa leo kwa upande wa Jamhuri kuleta mashahidi, ambapo Wakili Asenga aliomba tarehe nyingine ya kusikilizwa kwa kesi hiyo kutokana na shahidi kupatwa na udhuru.
Aidha ameiomba Mahakama kuwapatia hati za wito mashahidi wa kesi hiyo.
“Mheshimiwa Hakimu kesi imepangwa kusikilizwa lakini shahidi amepatwa na udhuru, hivyo tunaomba tarehe nyingine ya kusikilizwa pamoja na hati za wito za mashahidi kuitwa mahakamani,”
Baada ya maelezo hayo Hakimu alihoji upande wa utetezi kama una hoja za kuhoji upande wa Jamhuri.
Wakili wa utetezi Owora ameieleza mahakama kuwa wamejiandaa kwa ajili ya kesi kusikilizwa na kwamba hawahijataji mambo ya kupotezeana muda huku akihoji kama leo upande wa jamhuri ulikuwa unaleta mashahidi iweje waombe mahakama iwape hati za wito kwa ajili ya mashahidi hao.
Na Lilian Joel