MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini, Inspekta Jenerali Simon Sirro, ameagiza zifanyike operesheni za kuwakamata wahalifu nchini wanaotumia pikipiki kupora na wale wanaojihusisha na uvunjaji na kuiba mali za wananchi.
Sirro ametoa agizo hilo jana alipofanya ukaguzi wa ghafla katika Kituo cha Polisi cha Stakishari, Tabata Shule na Kawe, Jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuona changamoto zilizopo vituoni hapo.
“Tumebaini kuna matukio ya pikipiki kupora kwa jina la mitaani wanajiita ‘vishandu,’ wameongezeka kwani mtu anashika mkoba wake dereva wa bodaboda anatoka nyuma na kukwapua.
“Matatizo mengine madogo yaliyopo ni uvunjaji usiku, ninaagiza operesheni za nguvu zifanyike kuhakikisha matukio haya yanapungua kwa kiasi kikubwa,” alisema.
Pia, aliwaomba wananchi kutoa msaada dhidi ya matukio hayo kwa sababu huwa yanapunguzwa kupitia ulinzi shirikishi.
Kutokana na hilo, Sirro aliwataka Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Watendaji Kata na Polisi Kata, kuendelea kuhamasisha vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuhakikisha matukio ya uhalifu yanapungua katika maeneo yao.
“Ni aibu ikifika muda wa usiku mnauacha mtaa bila ulinzi kisa askari, hatutoshi ni lazima tushirikiane kuhakikisha uhalifu wa uvunjaji unapungua, lakini wa ‘vishandu’ lazima tufanye operesheni kubwa zaidi ili tupate taarifa kwa wananchi,” alisema.
Pia, Sirro aliwataka madereva hasa wa pikipiki maarufu kama bodaboda, kufuata masharti ya leseni zao na kuacha kujiingiza katika matukio ya uhalifu wa kutumia nguvu.
“Mmeshapata leseni na mnafanya kazi halali ya kubeba abiria, unapojiingiza katika kazi mbaya ya unyang’anyi wa kutumia nguvu yatakayokupata usije kulalamikia Jeshi kwa sababu unachofanya sicho ulichoelekezwa katika leseni yako.
“Unaacha kazi ya kubeba abiria unasema hailipi na inayolipa ni kupora mikoba ya akina mama, nikuhakikishie hautachukua muda mrefu utapata matatizo na baadae usije lilaumu Jeshi la Polisi,” alisema.
Sirro alisema kwamba, Jeshi la Polisi lipo vizuri na matukio ya uhalifu yanazidi kupungua, hivyo aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za kihalifu ili kuhakikisha nchi inakuwa salama.
Na ATHNATH MKIRAMWENI