MKAZI wa Kijiji cha Ng’wabasabi, Kata ya Nyehunge, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, Juma Gervas (21), anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 66 (jina linahifadhiwa).
Akizungumza na UhuruOnline, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng’anza, alithibitisha kutokea tukio hilo, Agosti 20, mwaka huu, saa nane usiku, katika Kijiji cha Ng’wabasabi, Halmashauri ya Buchosa.
Alisema mtuhumiwa baada ya kufanya unyama huo alitoroka ambapo baada ya msako polisi walimkamata akiwa mafichoni. Alieleza kuwa siku ya tukio, mtuhumiwa alikwenda nyumbani kwa mwanamke huyo saa nane usiku kisha kuvunja mlango kwa kutumia panga na kuingia ndani.
“Baada ya kuingia ndani alimkamata mwanamke huyo na kumziba mdomo kwa kutumia mkono ili asipige kelele, kisha akambaka na baada ya kutimiza tendo hilo la kikatili, alitoweka,” alieleza.
Kamanda huyo wa polisi alisema taarifa ilitolewa Kituo cha Polisi Nyehunge kuhusu kutokea tukio hilo, ambapo uliitishwa mkutano wa hadhara kujadili na namna ya kumtia mbaroni mtuhumiwa ambaye alifahamika kupitia kwa mtoa taarifa.
“Askari walifanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo na upelelezi wa tukio hilo umekamilika na tayari amefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Sengerema kujibu tuhuma hizo,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ng’abasabi, Daud Nomolomo, alisema matukio ya ukatili likiwemo la mama huyo kubakwa hayapaswi kufumbia macho na jamii.
“Baada ya tukio hilo kutokea tuliitisha mkutano wa hadhara wa kijiji kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari, madhara ya ukatili na ubakaji, hatima ya watuhumiwa ni kifungo jela au kufungwa maisha kulingana na uzito wa kosa kisheria,”alieleza.
Mwenyekiti huyo alisema ulinzi wa raia na mali zao ni jukumu la kila mwananchi, hivyo, viongozi wa serikali ya kijiji wameanzisha ulinzi shirikishi ili kudhibiti uhalifu ikiwemo kuwakagua wageni wanaoingia kijijini hapo.
Naye, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Christian Aloys, alisema watu wanaotuhumiwa kwa vitendo vya ubakaji katika jamii, wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria bila kuonewa huruma ili liwe fundisho kwa wenye tabia za namna hiyo.
Na BALTAZAR MASHAKA, Sengerema