ULE MSEMO WA KWAMBA ELIMU HAINA MWISHO NI HUU… KWA kile kinachoonekana si kitu cha kawaida kutokea kwa jamii Bibi aitwaye Kezia Mashingia (75) Mkazi wa Moshi kesho Novemba 27, 2021. anahitimu masomo yake ya shahada ya uzamivu (PhD) katika chuo kikuu Cha kikatoliki Mwenge (MweCau).
Bibi Kezia ambaye ni Mama wa watoto 8 na wajukuu 15 anasema aliamua kujiendeleza kimasomo baada ya kustaafu kazi rasmi serikalini akiwa na miaka 60 na akaendelea kufundisha katika chuo hicho huku akiwa anajiendeleza kimasomo kwa ngazi tofauti tofauti.
“Wakati naanza kufanya kazi nilikiwa na elimu ya shahada ya kwanza lakini pia nilikuwa na ndoto zakujiendeleza kimasomo jambo ambalo naona limefanikiwa licha ya kuwa tayari nina umri mkubwa “alisema
Amesema alipomaliza elimu ya msingi 1966 alijiunga na shule ya sekondari ya wasichana Tabora kati ya mwaka 1967-1968 na hatimaye alihitimu na kujiunga na jeshi mwaka 1969.
Amesema baada ya hapo alijiunga na chuo kikuu mwaka 1972 akasoma astashahada ya uzamili katika elimu na alipohitimu akafanikiwa kufanya kazi katika vyuo mbalimbali vya elimu ikiwemo Mpwapwa, Chang’ombe Sekondari ya Makumira na Vunjo.
“Huko kote nilikuwa nazunguka kufuata mume wangu ila nikahamia chuo hiki kikuu Cha Kikatoliki Mwenge hadi 2006 nilipostaafu mwaka 2006 nikiwa na miaka 60” alisema
Alisema baada ya kustaafu alijiunga na chuo kikuu huria kwa masomo ya astashahada kwa kipindi cha miaka 2 na alipohitimu akajiunga na shahada ya uzamili katika chuo Kikatoliki cha Mwenge.
Kwa mujibu wa Bi Kezia ni kuwa alijiunga tena na chuo hicho kwa masomo ngazi ya shahada ya uzamivu akiwa na umri wa miaka 70 na kuwa sasa anaenda kuhitimu huku kiu yake ikiwa ni kuanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kuwasaidia wasichana na wanawake kupata elimu.
Afisa uhisiano wa chuo kikuu Kikatoliki cha Mwenge (MweCau), Atanas Sing’ambi, amesema Kezia ni mmoja Kati ya wanafunzi 5 wanaoenda kuhitimu ngazi ya shahada ya uzamivu katika mahafali hayo ya 14 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho.
Amesema katika mahafali hayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Shinyanga, Askofu Liberatus Sangu, huku jumla ya wahitimu 851 wanaenda kuhitimu katika ngazi mbalimbali.
“Ngazi ya astashahada 73, stashahada 145, shahada ya kwanza 570 astashahada ya uzamili 20, shahada ya uzamili 38 na shahada ya uzamivu ni 5” alisema
Na Gift Mongi, Moshi