LEO ni siku ya 365 zinazounda mwaka mmoja tangu Rais Samia Suluhu Hassan, aapishwe kushika wadhifa wa urais, huku maeneo ya usawa wa jinsia, elimu na afya, yakitajwa kuwa vielelezo vya ufanisi katika uongozi wake.
Ilikuwa Machi 19, 2021, alipoteuliwa kushika wadhifa huo baada ya kifo cha mtangulizi wake Hayati Dk. John Magufuli kilichotokea Machi 17, mwaka jana.
Kuapishwa kwake kuwa rais kumemfanya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa mkuu wa nchi tangu uhuru wa Tanganyika, hivyo kuwa turufu katika juhudi za kupigania usawa wa jinsia.
Mwaka mmoja wa uongozi wake, umerekodi mafanikio lukuki katika usawa wa jinsia, sekta ya elimu na afya, huku wadau wakimsifu kwa kusema ni kielelezo cha uwezo wa wanawake katika uongozi.
Usawa wa jinsia
Katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake, Rais Samia ameifanya Tanzania kuwa mwamba wa utekelezaji wa dhana ya usawa wa jinsia katika ngazi za uamuzi.
Ndani ya kipindi hicho, imeshuhudiwa idadi kubwa ya wanawake, walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali, zikiwemo nyeti kama Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambapo waziri wake ni Dk. Stergomena Tax.
Kwa mujibu wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN-WOMEN), Baraza la Mawaziri la Tanzania kwa sasa lina mawaziri tisa wanawake, idadi ambayo ni kubwa kuwahi kutokea katika mabaraza yote tangu uhuru wa Tanganyika.
Mbali na Baraza la Mawaziri, Rais Samia amekwenda mbali zaidi wakati wa uteuzi wa Majaji ambapo idadi ya wanawake ni asilimia 43.5.
Maeneo mengine yanayoashiria rasharasha za Tanzania kuelekea katika usawa wa jinsia katika ngazi za uamuzi ni idadi ya wabunge wanawake ambao ni asilimia 36, wakuu wa mikoa asilimia 30 na wakuu wa wilaya ni asilimia 15.
Haikuishia hapo tu, hata katika sekta binafsi kumekuwa na matokeo chanya katika usawa wa jinsia ambapo asilimia 30 ya wanawake katika kipindi hicho, wanaongoza taasisi za sekta hiyo.
Hata hivyo, uwepo wake madarakani umeongeza imani ya jamii kwa wanawake, kadhalika wanawake wenyewe kujiamini.
“Tulikuwa tunazungumza wanawake wanaweza bila ushahidi lakini uwepo wa Rais Samia umekuwa mfano wa uwezo wa wanawake, hii imeturahisishia kufanya harakati za usawa wa jinsia,” alisema Rebecca Gyumi, Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Iniative.
Shirika hilo la UN-WOMEN, linabainisha ulimwenguni ni wanawake 26 pekee ndiyo walioshika wadhifa wa urais, akiwemo Rais Samia wa Tanzania.
Kwa sasa ni nchi 10 pekee ndiyo zenye wakuu wa nchi wanawake ambapo Tanzania ni miongoni mwazo.
“Bahati nzuri Tanzania kwa Afrika imekuwa miongoni mwa nchi hizi 10 zenye wakuu wa nchi wanawake, hiki ni kielelezo cha maendeleo katika usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake,” alisema Hodan Addou, Mwakilishi wa UN-Women.
Mwamko wa ongezeko la wanawake katika ngazi za uamuzi umeendelea kushika kasi katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia, kwani kwa sasa Mhimili wa Bunge, unaongozwa na mwanamke.
Dk. Tulia Ackson anakuwa mwanamke wa pili kushika wadhifa wa Spika wa Bunge huku mwanamke wa pili kuongoza mhimili ambapo wa kwanza ni Rais Samia anayeiongoza serikali.
Pamoja na mafanikio ya ongezeko la wanawake katika uongozi, pia kumekuwa na maboresho mengine yaliyofanyika kutanua wigo wa fursa kwa wanawake kuyafikia mafanikio.
Kuhusu hilo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dk. Zena Mabeyo, alisema kupitishwa sheria inayowaruhusu watoto walioacha shule kutokana na changamoto mbalimbali kurudi shuleni ni moja ya mafanikio muhimu katika kipindi hicho.
Alifafanua hatua hiyo imeongeza fursa hasa kwa watoto wa kike kupata elimu, ambayo kabla walikosa kutokana na changamoto walizopata ikiwemo kubakwa.
Dk. Zena alisema hiyo itasaidia watoto wa kike kuzifikia ndoto zao na kuwa mama bora wa familia, kwani wengi walijifungua wakiwa wadogo na kwa sababu wanakosa kusoma, hawakuwa na ujuzi wa malezi.
“Angalau wanarudi shuleni watapata elimu juu ya malezi hivyo tunawaandaa kuwa mama bora, lakini sio hivyo tu, hata ile hatua ya kuendelea na masomo wanaongeza maarifa yatakayowawezesha kusaidia watoto wao baadaye,” aliongeza Dk. Zena.
Dk. Zena alisema hatua ya Rais Samia kutoa nafasi za uongozi kwa wanawake, itasaidia kufikia usawa na kupunguza tofauti kati ya wanaume na wanawake katika uongozi, jambo ambalo lina faida lukuki katika jamii.
SEKTA YA ELIMU
Katika kipindi hicho, sekta ya elimu imepitia mapinduzi makubwa hasa ya uboreshaji wa miundombinu ya madarasa.
Kupitia fedha za mkopo wa masharti nafuu sh. trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF), kiasi cha sh. bilioni 304 zilitumika kujenga miundombinu ya madarasa.
Fedha hizo zimewezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa 13,000 ya shule za sekondari na sh. bilioni 60 kujenga Vituo Shikizi nchini na hivyo kuwezesha wanafunzi 600,000 kupata vyumba vya kusomea.
Utekelezaji wa miradi hiyo umefanikisha kukoma kwa changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa kwa asilimia 100 katika shule za sekondari, ambao awali ulisababisha wanafunzi kuingia madarasani kwa awamu.
Ujenzi wa vyumba hivyo umewezesha wanafunzi 135,000 kupata vyumba vya madarasa bora ambapo ukamilishwaji huo umeenda sambamba na ununuzi wa madawati 45,000.
Hata hivyo, upatikanaji wa fedha hizo kutoka IMF ni matokeo ya juhudi zake za kuimarisha ushirikiano na uhusiano na mataifa ya nje na jumuiya za kimataifa.
AFYA
Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia kumekuwa na uimarishwaji wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.
Asilimia 99.7 ya wajawazito walifanya mahudhurio manne au zaidi katika kipindi, ikilinganishwa na asilimia 85.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.
Aidha, asilimia 81.5 ya wajawazito walijifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya, ukilinganisha na asilimia 80 waliojifungulia vituo vya kutolea huduma kwa kipindi kama hicho mwaka 2020.
Utoaji wa chanjo kwa watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja ulikuwa asilimia 97 kwa kutumia kigezo cha PENTA-3.
Chanjo hizo ni kwa ajili ya kuzuia magonjwa ya dondakoo, kifaduro, pepopunda, homa ya ini na homa ya uti wa mgongo hivyo kuvuka kiwango cha asilimia 90 kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ikilinganishwa na asilimia 95 iliyokuwa imefikiwa mwaka 2020.
Katika kuboresha sekta hiyo, Rais Samia ndani ya mwaka mmoja alitoa sh. bilioni 226.68 kwa ajili ya huduma za afya ya msingi.
Aidha vipaumbele vilivyotekelezwa kupitia fedha hizo ni kuanzisha Huduma za Dharura (EMD) katika halmashauri 75 na kujenga majengo ya huduma za wagonjwa mahututi 25 katika Halmashauri 25 za kimkakati.
Kuhusu hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mbilinyi, alisema huduma hizo ni msingi mzuri katika kuongeza ustawi wa binadamu.
Alisema iwapo binadamu watakuwa na ustawi maana yake afya za akili na miili yao zitaimarika na hivyo kuwa na mchango chanya katika uchumi wa nchi.
Alisisitiza kwamba maboresho ya huduma za mama na mtoto katika Hospitali mbalimbali nchini ni moja ya hatua zinazoonesha msisitizo wa Rais Samia katika kuwaondoa wanawake katika wimbi la changamoto.
JUMA ISSIHAKA NA IRENE MWASOMOLA