TAKRIBAN vijana 4,000 wa mikoa ya Dodoma, Lindi na Manyara wanatarajia kunufaika na mafunzo maalumu ya ufundi stadi yatakayowapa ujuzi na utayari wa kuajiriwa au kujiajiri, kupitia mradi wa Ajira na Ujuzi kwa Maendeleo ya Tanzania.
Makubaliano ya utekelezaji wa mradi huo yametiwa saini Juni 28, mwaka huu, jijini Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk. Pancras Bujulu na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Korea (KOICA) nchini Tanzania, Kyucheol Eo.
Akizungumza wakati wa kutia saini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkazi wa KOICA hapa nchini, Kyucheol Eo, amesema serikali yake imetenga kiasi cha Dola za Kimarekani 5,300,000 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na kwamba utatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia 2021 hadi 2023.
Amesema VETA itashirikiana kwa karibu na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ) katika utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha vijana wa kitanzania wananufaika na ukuaji wa uchumi katika sekta zinazotegemea ujuzi wa ufundi stadi.
“KOICA inafurahi kushirikiana na VETA kusaidia vijana nchini Tanzania kupata ajira ikiwa ni pamoja na kujiajiri ili waweze kutimiza ndoto zao. Tutashirikiana pia na GIZ kutekeleza mradi huu ambao utanufaisha moja kwa moja vijana 4,000, ambapo kati yao 1,400 ni wanawake,” amesema Kyucheol.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk. Pancras Bujulu, ameishukuru Serikali ya Korea kwa ufadhili huo na kusema kuwa mradi huo umejikita katika kutoa mafunzo ya muda mfupi kwenye fani za Uchomeleaji (Welding), Ufundi Bomba wa Viwandani (Industrial Plumbing) na Mekatroniki (Mechatronics).
Amesema mradi huo, pamoja na mambo mengine, utawapatia vijana hao mafunzo ya ujasiriamali na kutoa fedha kama mtaji ili kuwawezesha wahitimu kuanzisha miradi yao na kuwawezesha kujiajiri.
Mitaji hiyo itatolewa kwa timu za wanafunzi zitakazoshinda kupitia uwasilishaji wa miradi bora itakayopatikana kupitia shindano maalum la ujasiriamali litakalofanyika kila mwaka.
Na Pius Ntiga