MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema hadi Juni mwaka huu, laini za simu za mkononi zilisosajiliwa zilifikia milioni 53.1 huku watumiaji wa huduma ya intaneti wakiwa milioni 29,1.
Kauli hiyo ilitolewa na Ofisa Mwandamizi Mkuu TCRA, Semu Mwakyanjala, alipozungumza na UhuruOnline katika maonyesho ya Afrika Mashariki ya wajasiriamali wadogo na wa kati yanayofanyika jijini Mwanza.
Alisema kasi ya mabadiliko hayo imeongezeka katika kipindi cha miongo mitatu ya mwisho ya kipindi cha sasa kwa sababu ya mabadiliko ya teknolojia duniani, sera, sheria, miongozo imara na usimamizi wenye weledi.
“Hadi Desemba 9, mwaka 1961, huduma za mawasiliano ya simu na posta zilisimamiwa na taasisi zilizokuwa chini ya mfumo wa ushirikiano miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki. Utangazaji uliendeshwa kwa utaratibu wa nchi husika, huduma za intaneti hazikuwepo kipindi hicho na zilianza kutolewa mwanzoni mwa miaka ya tisini,” alisema.
Alisema baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuvunjika mwaka 1977, kila nchi iliweka utaratibu wa kuziendesha ambapo Tanzania ilianzisha Shirika la Posta na Simu (TP&TC), lililotoa huduma na kusimamia sekta ndogo ya mawasiliano ya simu na posta.
Mwakyanjala alisema Desemba, mwaka 1993, TP&TC ilivunjwa zikaundwa taasisi tatu, kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Tume ya Mawasiliano (TCC) na Tume ya Utangazaji (TCC).
Alibainisha kuwa kutokana na mwelekeo wa teknolojia, tume hizo mbili ziliunganishwa na kuanzishwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
“Kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia duniani ambayo yaliwezesha huduma mbalimbali za mawasiliano kuwa changamani, mwaka 2005 serikali kupitia TCRA ilianzisha mfumo mpya wa leseni usiotegemea teknolojia au huduma fulani,”alieleza.
Kwa mujibu wa Mwakyanjala, mfumo huo ulichangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kasi ya maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini.
Alibainisha kuwa kwa sasa wenye leseni za kuweka miundombinu ni 23, leseni za simu za mkononi na mezani 10, (kampuni saba zinatoa huduma),leseni za huduma tumizi za mawasiliano 79, redio 205 na televisheni 51 zinazorusha matangazo bila kulipia.
Mwakyanjala alisema kuwa mwaka 2006 serikali ilianzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ili kuharakisha kasi ya kuenea huduma za mawasiliano kwenye maeneo yasiyofikika kwa kirahisi na yasiyovutia kibiashara.
Alieleza kuwa sekta ndogo ya posta haikuonyesha maendeleo makubwa hasa kuanzia muongo wa nne wa miaka 60 ya Uhuru kutokana na kushuka kwa biashara yakawaida ya posta iliyochangiwa na maendeleo ya teknolojia.
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza