MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Mkoa wa Kilimanjaro, imeyakamata magari 212 kuanzia Julai hadi Septemba, mwaka huu kutokana na makosa ya ukiukwaji wa leseni za usafirishaji na kanuni zake.
Akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa Mfawidhi wa LATRA, Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Nyello, alisema kukamatwa kwa magari hayo ni matokeo ya taarifa kutoka kwa wasafiri na watumiaji wa vyombo hivyo kuhusu ukiukwaji wa sheria.
“Tunasimamia sheria na hii operesheni iliyofanywa kwa miezi mitatu itakuwa endelevu, watu wasidhani ni nguvu ya soda. Jambo la msingi ni wasafirishaji kufuata utaratibu wa leseni na si vinginevyo.
“Magari hayo yamekamatwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo kukatisha safari bila kufuata sheria, kuingia njia ambazo haziwahusu, kutoza nauli tofauti na ile elekezi na lugha chafu kwa abiria,”alisema.
Nyello alieleza kuwa baada ya kuyakamata magari hayo, wamiliki walitozwa faini kwa mujibu wa sheria ili wajifunze kuzingatia sheria.
Kutokana na operesheni hiyo, LATRA Mkoa wa Kilimanjaro imewaonya baadhi ya madereva wanaokiuka sheria kwamba watachukuliwa hatua za kali.
Akizungumzia operesheni hiyo, Mkazi wa Kibosho, Gerald Mmasy, alisema kwa sasa wamiliki wa magari ya kusafirisha abiria Moshi-Kibosho wamekuwa wakipandisha nauli kiholela hususan nyakati za usiku.
“Operesheni inayoendeshwa na LATRA huenda itakwenda kuondoa adha tuliyokabiliana nayo kwa kipindi kirefu. Ni vema wasafiri tukawa kitu kimoja kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi tunapoona kuna viashiria vya uvunjwaji wa kanuni au sheria za usafirishaji kwa maksudi,” alieleza.
Na Gift Mongi, Moshi