WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amewataka wakuu wa mikoa nchini, kuhakikisha wanasimamia na kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika mikoa yao.
Amesema wakuu wa mikoa hao wanapaswa kuchukua hatua hizo kwa kuwa kazi ya kamati ya Mawaziri wanane wa Wizara za kisekta ni kushughulikia migogoro ya vijiji 975.
Lukuvi ameyasema hayo mkoani humo, alipozungumza na viongozi, wabunge na watendaji wengine wakati wa ziara ya mawaziri wa kisekta.
Amesisitiza kuwa, kamati ya mawaziri wanane kazi yake kubwa ni kuangalia vijiji 975, lakini mkoa unatakiwa kusimamia kazi ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, kwa kuwa taarifa iliyopatiwa kamati inawezekana siyo ya migogoro yote ya matumizi ya ardhi katika mkoa.
“Kamati yetu ya mawaziri wanane itaendelea kwa vile vijiji 975, ila kazi ya kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi itaendelea kwa usimamizi wa wakuu wa mikoa na kama ipo sababu ya msingi ya kuondoa baadhi ya vijiji, basi mkoa utainisha kwa kuwa kilichofanyika sasa hivi ni huruma ya Rais” alisema Lukuvi.
Alifafanua kuwa kila mkoa mawaziri wanane wa Wizara za Kisekta wanapopita wanaacha tume ya wataalamu ili kuangalia namna bora ya utekelezaji uamuzi wa Baraza la Mawaziri kuhusu migogoro ya ardhi katika vijiji kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Kila kamati yetu inapopita katika mikoa kuna taarifa mpya kuhusu migogoro ya matumizi ya ardhi, hivyo wakuu wa mikoa wana jukumu la kuhakikisha migogoro ya matumizi ya ardhi katika mikoa yao inakoma na haijirudii tena,” alisisitiza.
Aliwataka wakuu wa mikoa nchini kusaidia katika suala hilo ili kero zote kuhusu migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji itatuliwe bila kuumiza wananchi na lazima iishe na kama mkoa ukihitaji kusaidiwa utoe taarifa na utekelezaji wake utafanyika kwa haraka.
Kwa mujibu wa Lukuvi kilichofanya kumega sehemu maeneo ya hifadhi ni huruma ya Rais Samia Suluhu Hassan na kusisitiza kuwa, kama eneo ni chanzo cha maji linahitaji kutunzwa.
Alisema ni aibu kuendelea kuwepo migogoro ya ardhi ikiwemo ya mipaka katika mikoa huku akitaka imalizwe kwa mfumo huo.
“Ni aibu kubwa kusikia kuna mpaka wa mkoa na mkoa au wilaya na wilaya kwa kuwa mwenye mamlaka ya kuweka mipaka ni rais na wakuu wa mikoa ninyi hamuendi kuanzisha mipaka mipya nendeni mkaweke alama kuwaonyesha wananchi,” alisema.
Baadhi ya wabunge wa mkoa wa Tabora, waliwasilisha kero za migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo yao kwa kamati ya mawaziri wanane kwa kusema baadhi ya wananchi wamekuwa wakiishi kwa hofu kwa kuelezwa wanaishi ndani ya hifadhi.
Mbunge wa Jimbo la Kaliua, Aloyce Kwezi, aliiambia kamati hiyo kuwa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA), imeweka mipaka ya hifadhi ya msitu wake wa USAWIWA hadi ndani ya mipaka ya vijiji na kuanza kuchukua hatua za kuwaondoa wananchi, jambo linalowafanya kuishi kwa hofu wakati wameishi hapo kwa muda mrefu.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja aligiza taasisi zilizoko chini ya wizara yake kuacha kuwasumbua wananchi wanaoishi maeneo ya hifadhi kipindi hiki ambacho kamati hiyo inazunguka katika mikoa mpaka pale itakapoamuliwa vinginevyo.
“Naomba tuvute subira wakati tunatekeleza uamuzi wa Baraza la Mawaziri kuhusu migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975. Kuna maeneo yamesahaulika na tume imeundwa na Waziri wa Malisili na Utalii kufanya tathmini kwa baadhi ya maeneo na kutaka wananchi waachwe katika maeneo wanayoishi wasibughudhiwe,” alisema.
Na Mwandishi Wetu, TABORA