MAADHIMISHO ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, yamefana jijini Dar es Salaam yakipambwa na vikosi vya gwaride na halaiki maalumu kutoka kwa watoto wa shule za msingi.
Aidha, maadhimisho hayo, yalikuwa ya aina yake katika Uwanja wa Uhuru ambao unaokadiriwa kuingia watu 23,000, uliokuwa umefurika na baadhi ya wananchi kulazimika kukaa Uwanja wa Mkapa.
Sherehe za maadhimisho hayo, zilianza saa 2:00 asubuhi huku kukiwa na utulivu ambapo onyesho la uokoaji lilifanywa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kufuatiwa na kwata ya Jeshi la Polisi kabla ya uhuru, waliovalia kaptura nyeupe, soksi ndefu nyeupe na kofia nyekundu.
Walipita kwa mwendo wa ukakamavu na haraka kuzunguka uwanja kuonyesha namna Jeshi la Polisi lilivyokuwa kabla ya uhuru huku mikononi wakishika fimbo
Wakati kwata inaendelea Rais mstaafu wa Malawi, Dk. Joyce Banda aliwasili uwanjani hapo saa 2:38 asubuhi huku wageni wengine waalikwa, viongozi wa serikali na wananchi wakiendelea kuwasili.
Saa 2:46 Rais wa Mahakama ya Afrika aliwasili huku gwaride la kimya kimya lililofanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likionyesha umahiri na maumbo mbalimbali ikiwemo nyota na namba 60 kuashiria maadhimisho hayo.
Baadaye Makamu wa Rais wa Msumbiji aliwasili na kisha Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na mwenza wake waliwasili saa 2:52.
Kwata ya kimyakimya ilipokamilika wasanii mbalimbali walipata fursa ya kutumbuiza katika sherehe hizo, wakitanguliwa na Bendi ya TOT.
Saa 3:03 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah na mwenza wake waliwasili na kufuatiwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete, kisha Naibu Waziri Mkuu wa Eswatini na mwenza wake waliowasili saa 3:07.
Dakika nane baadaye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Kitaifa aliwasili uwanjani hapo akiwa na mwenza wake kisha kufuatiwa na Makamu wa Rais wa Burundi, Prosper Banzumbanja, aliyewasili saa 3:16.
Alifuata ni mjane wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, mama Maria Nyerere aliyewasili saa 3:20 na kufuatiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, mwenza wake na Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi waliowasili saa 3:25.
Sherehe hizo zilizopambwa kwa nakshi za mabango yaliyoandikwa ‘MIAKA 60 YA UHURU Tanzania Imara, Kazi Iendelee’ ikiwa ndiyo kauli mbiu ya sherehe hizo, zilihudhuriwa na wajane wa waasisi wa taifa ambao ni Mama Maria Nyerere na Mama Karume wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.
Viongozi waliendelea kuwasili ambapo saa 3:30 Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango aliwasili na mwenza wake, kisha tarumbeta kupigwa kuashiria gwaride kuingizwa uwanjani.
Wakati gwaride linaendelea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) aliwasili saa 3:33 na kisha gwaride kuanza kuingia uwanjani.
Kuingia kwa gwaride kuliamsha hisia za wananchi wengi uwanjani hapo ambapo waliibua shangwe, nderemo na vifijo huku vikosi vya majeshi vilivyojigawa kwa makundi 13 vikiingia kutoka pande zote za uwanja kwa mpangilio maalumu wakionyesha mwendo wa madaha na ukakamavu huku kila kikosi kikiwa kimevalia sare zake.
Aidha, kikosi cha bendera chenye askari watano kiliingia uwanjani na hivyo wananchi na askari kusimama kutoa heshima, huku ushiriki wa Jeshi la Uhamiaji ambalo ni mara ya kwanza kuwa katika gwaride na maonyesho hayo kwa ujumla ikiwa ni kivutio.
Saa 3:53 mwenza wa Rais wa Tanzania, Hafidh Ameir, aliwasili kwa gari aina ya BMW na kufuatiwa na Rais wa Visiwa vya Comoro, Azali Ousumane aliyeingia uwanjani hapo saa 3:55.
Msafara wa mwenza wa Rais Samia, ulifungua kuwasili kwa wakuu wa nchi ambapo Rais wa Msumbiji, Felipe Nyusi, aliwasili saa 3:56.
Mnamo saa 3:57 aliwasili Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na saa 4:01 aliwasili Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ambapo wananchi waliibua shangwe na vigelegele wakimshangilia.
Rais Samia, aliwasili uwanjani hapo saa 4:18 akiwa amebebwa katika gari maalumu la wazi na kuzungushwa uwanjani kwa dakika nne huku akisalimia kwa kupungia wananchi mkono katika kila upande.

Shangwe ziliibuka katika kila jukwaa alilokaribia uwanjani hapo, huku akionekana nadhifu akiwa amevalia mtandio mwekundu na suti nyeusi na kama ilivyo kawaida yake akitoa tabasamu kuashiria kufurahishwa na sherehe hizo.
Aliposhuka alikwenda katika jukwaa maalumu saa 4:23 kuruhusu wimbo wa taifa kupigwa na wimbo wa Afrika Mashariki huku mizinga 21 ikipigwa.
Saa 4:27 Rais Samia alianza kukagua gwaride kwa mwendo wa ukakamavu akisindikizwa na wimbo wa ‘Tanzania Tanzania’ kitendo kilichofanyika kwa dakika 10 na kisha akapanda jukwaa kuu kuungana na viongozi wenzake.

Saa 4:38 gwaride lilianza kuchezwa kwa mwendo wa polepole kuzunguka uwanja likionyesha ukakamavu na umahiri likisindikizwa na Brass Band ya JWTZ na kisha mwendo wa haraka.
Madaha ya majeshi hayo katika kuchezea silaha wakati wa gwaride, ndilo jambo lilioonekana kukonga nyoyo za wengi waliohudhuria sherehe hizo kwani wakati wote walipiga makofi na kushangilia.
Gwaride hilo lilifanyika kwa dakika 50 na kisha saa 5:18 askari kikosi cha wanamaji waliobeba mizigo yenye uzito wa kilo 30 walipita na kutoa heshima kwa Rais huku wakiwa wamevalia sare nyeusi.
Baada ya kikosi hicho, wengine waliopita ni askari wa wana maji waliobeba mabegi yenye uzito wa kilo 50 ndani yakiwa na vitu vya kuwasaidia kuishi kwa siku kadhaa wanapokuwa vitani.
Saa 5:27, gwaride lilimalizika na kutoka uwanjani ili kuruhusu ratiba nyingine ziendelee.
Aidha saa 5:35, watoto wa halaiki walionekana kuwa kivutio zaidi katika sherehe hizo kwa kuonyesha matukio ya kutengeneza maumbo ikiwemo ya miaka 60 ya Uhuru, kusisitiza uimara wa Jeshi la Tanzania na umuhimu wa afya njema kwa taifa.

Pia, walionyesha matukio ya kudhibiti moto, jinsi ya kutumia silaha wakiwa vitani, namna waasisi ya taifa walivyojitoa katika kupigania Uhuru na michezo mbalimbali.
Watoto hao walitumia fursa hiyo, kutoa salamu na ujumbe uliosisitiza miaka 60 ya Uhuru Tanzania Imara Kazi Iendelee na kuimba wimbo maalumu ukieleza kuwa ni furaha kwa kila mtanzania kuzaliwa katika taifa hili lenye utamaduni, umoja na mshikamano.
Saa 6:51, yalianza maonyesho ya askari wakiwa wamevalia mavazi ya vikosi vya zamani kabla ya uhuru, yaliyofanywa na JWTZ.
Askari hao walivalia mavazi ya kaptura zenye rangi ya kaki na kofia huku wakiwa pekupeku, mavazi yaliyovaliwa miaka ya nyuma kabla ya uhuru.
Pia walionyesha mavazi ya Jeshi la Ulinzi kwa sasa, Jeshi la akiba na vijana wa skauti.
Awali, jeshi lilionyesha namna watumishi wake wanavyoweza kubeba mizigo ya kuanzia kilo 30, 50 na 100 wakiwa vitani na silaha ambao walipita mbele ya umati wa watu katika sherehe hizo.

Saa 7:00 zilipita ndege mbili kwa ajili ya usafirishaji aina ya helikopta huku onyesho la silaha, zana za kivita likiendelea mbele ya Rais na wakuu wengine wa nchi za Afrika waliohudhuria sherehe hizo.
Wakati huo ndege nyingine ya usafirishaji wa vifaa mbalimbali vya kijeshi na kutoa msaada wa kiraia ilipita.
Miongoni mwa silaha hizo zilikuwepo zinazompiga adui aliyejichimbia katika handaki, kombora la kuharibu ngome ya silaha za adui, vifaru, mizinga inayotumika kupiga adui wa wazi.
Onyesho lililowaduwaza wengi ni kifaru chenye uwezo wa kupita katika maji na nchi kavu ambacho hutumiwa na jeshi la wana maji.
Pia, jeshi lilitumia maonyesho hayo kuonyesha daraja lenye uwezo wa kujengwa na kutenguliwa kwa muda wa dakika 20 na jingine dakika 60.
Kadhalika zilionyeshwa silaha za kutungulia ndege za adui inayopita kimo cha chini huku ndege tatu za mafunzo ya kivita zikipita.
Pia, kilionyeswa kikundi cha mbwa vita ambao kazi yao ni kukamata na kushambulia maadui, kutegua mabomu na kusaka zilipo silaha za adui.
Saa 7:15 zilipita ndege vita tatu zikiwa katika mwendo kasi, baadaye ndege moja ilipita kwa kasi zaidi, nyingine mwendo wa kujiviringisha na ya mwisho ilipita ikitoa heshima kwa Rais.
Saa 7:29 macho yaligeukia kaskazini mwa uwanja ilipokuwa inatokea helikopta ya uokoaji ya JWTZ, ambazo zilishusha askari kwa kamba na kuonyesha namna wanavyoweza kutua kwa kasi na kunyakuliwa kwa kamba huku wakipepea bendera ya taifa tukio lililoamsha furaha kwa wananchi wakionyesha kuridhishwa na namna jeshi lilivyojidhatiti katika ulinzi na usalama.
MARIAM MZIWANDA NA JUMA IS’HAKA