WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amekemea tabia na majitaka kutoka viwandani na katika migodi, kwani inachangia kuhatarisha usalama wa afya ya binadamu na mazingira.
Pia, ametoa maagizo 15 kwa wizara, taasisi na mamlaka za serikali za mitaa kuhusu uhifadhi wa mazingira nchini, akataka yatekelezwe kikamilifu.
Alitoa onyo hilo wakati akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kitaifa yalifanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
“Hivi karibuni, tumeshuhudia kutoweka kwa baadhi ya viumbe hai, maeneo mengi ya vyanzo vya maji yameathirika kutokana na ukame wa mara kwa mara, uchafuzi wa mazingira unaotokana na majitaka na kemikali kutokana na shughuli za viwandani.
“Uchafuzi huu, umeendelea kuongezeka kwa kasi nchini na kuathiri maji, hewa na ardhi. Hali hii, inahatarisha usalama wa afya ya binadamu na mazingira,” alisema.
Waziri Mkuu alikemea tabia ya uchomaji miti, uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu, ukataji miti holela kwa ajili ya uchomaji mkaa, uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji na uchomaji moto misitu.
Alisema kutokana na kuongezeka kwa uharibifu wa mazingira, aliiagiza wizara na taasisi husika na wananchi kwa ujumla, kuimarisha ushirikiano katika kukomesha uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu kote nchini.
Majaliwa aliwasihi wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha wanarejesha misitu, ikolojia na uoto wa asili katika maeneo yao ambayo miti ya asili iko katika tishio la kutoweka na kuwataka wawe walinzi wazuri wa mazingira kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho.
Waziri Mkuu alitoa maagizo 15 kwa wizara, taasisi na mamlaka za serikali za mitaa kuhusu uhifadhi wa mazingira nchini na kutaka yatekelezwe kikamilifu.
Akizungumza na washiriki wa maadhimisho hayo kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, Waziri Mkuu alisema Wizara ya Fedha na Mipango, inapaswa ihakikishe Mpango Kabambe wa Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira, unakuwa sehemu ya vipaumbele vya bajeti kila yaliyoharibiwa kwa kupata tena miti.
“Kila mamlaka ya serikali za mitaa, ihakikishe maeneo yote yaliyoharibiwa yanarejeshwa kwa kupandwa miti upya na kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa, ihakikishe inatekeleza vyema programu ya kitaifa ya upandaji miti 1,500,000 ili kuhakikisha nchi inakuwa ya kijani,” alisisitiza
Alizitaka wizara, taasisi, mashirika ya serikali na binafsi yanayotumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia au shughuli nyingine za uzalishaji, zianze kutumia nishati mbadala na kila mamlaka ya serikali za mitaa, ihakikishe inadhibiti matukio ya uchomaji ovyo misitu.
Kuhusu tafiti za nishati mbadala na viumbe wavamizi, alizitaka taasisi za utafiti na vyuo vya elimu ya juu, kufanya tafiti za nishati mbadala ili kuondokana na utegemezi wa nishati ya kuni na mkaa kwa kupikia.
Vilevile, alitaka zifanyike tafiti za namna ya kuzuia na kudhibiti kuenea kwa viumbe vamizi vinavyochangia uharibifu wa mazingira nchini.
Kuhusu takataka, amezitaka mamlaka za serikali za mitaa ziweke utaratibu wa kuhakikisha taka zinatenganishwa na zinakusanywa na zile zinazohusika na usimamizi wa mifereji ya maji ya mvua mijini, kuhakikisha inasafishwa ili kupunguza mafuriko.
Kuhusu misitu na uoto wa asili, Majaliwa alisema kila mamlaka ya serikali za mitaa, ihakikishe maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya misitu ya mijini katika mamlaka zao, hayabadilishwi matumizi wala kuvamiwa.
“Sekta zinazohusika zihakikishe kuwa ardhi na uoto asili katika vyanzo vya maji, vilima na milima iliyo katika maeneo yao inalindwa na kuhifadhiwa ili kuzuia mmomonyoko wa udongo na kukauka kwa vyanzo hivyo vya maji,” alisisitiza kuwa vilima vinavyozunguka mji wa Dodoma vihifadhiwe.
Kuhusu kilimo cha umwagiliaji, Waziri Mkuu alizitaka sekta zinazohusika na usimamizi wa shughuli za umwagiliaji mashamba, zihakikishe kunakuwa na matumizi sahihi ya maji yenye kuzingatia uhifadhi na ulinzi wa mazingira.
Pia, hifadhi za wanyamapori nazo, alizitaka mamlaka zinazohusika na usimamizi wa hifadhi, zidhibiti matukio ya ajali za barabarani kwa wanyamapori.
Vilevile zidhibiti shughuli za binadamu na uvamizi katika maeneo ya mapito ya wanyamapori (shoroba) ili kupunguza uharibifu wa mazao, mali na binadamu kupoteza maisha kutokana na kuwepo mwingiliano wa wanyama na binadamu.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Dk. Suleiman Jafo, alisema ofisi yake imezindua mpango wa soma na mti ambapo kila mwanafunzi anapaswa kupanda mti mmoja.
“Tumezindua kampeni ya Soma na Mti ambapo wanafunzi milioni 14.5 kutoka shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu wameshiriki kwa kupanda mti mmoja mmoja.
Waziri Mkuu alizindua Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira na kutoa tuzo kwa Mabalozi wa Mazingira na viongozi wakuu watano akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni Tanzania ni moja tu, Tunza Mazingira.
Na SELINA MATHEW, Dodoma