>> Ataka Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini kitoe elimu kwa waendesha Bodaboda aagiza trafiki wawe msaada kwa wananchi badala ya kero ili kuepusha ajali
Na JUMA ISSIHAKA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa maagizo saba kwa Jeshi la Polisi akilitaka liwe msaada na kimbilio la watumiaji barabara badala ya kuwa kero na chanzo cha ajali.
Amelitaka Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani kuelekeza semina zake zaidi kwa madereva wa Bodaboda, akisema ndiyo wanaotajwa kuwa vinara wa matukio ya ajali barabarani.
Rais Samia aliyasema hayo, Novemba 23, 2021, wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama jijini Arusha, iliyobeba kaulimbiu isemayo: ‘Jali Maisha Yako na ya Wengine Barabarani.’
Alisema miongoni mwa mbinu za kupunguza au kukomesha matukio ya ajali za barabarani ni Askari wa Usalama Barabarani kuwa msaada kwa wananchi badala ya kero.
“Askari wetu wawe msaada kwa wananchi na sio kero, wananchi wakiwaona wawakimbilie na sio wawakimbie kwa sababu ajali nyingine zinatokana na hawa vijana wetu wenye pikipiki, akiona unifomu anakata kichochoro huko anakokwenda hajui kuna nini ajali zinatokea,” alisema.

Aliwataka kuwa rafiki na wanaofanya nao kazi na kimbilio la wanaotumia barabara.
Alibainisha kero zinazotajwa kusababishwa na askari hao zikiwemo kushikilia leseni za madereva kwa muda mrefu, kulazimisha kulipwa faini papo hapo ilhali sheria inampa muda dereva kulipa faini hiyo.
Aliitaja kero nyingine kuwa ni idadi kubwa ya vyombo vya usafiri ambapo imeshuhudiwa katika Vituo vya Polisi kukiwa na Pikipiki nyingi zilizokamatwa hivyo, alilitaka jeshi la polisi kuliangalia hilo.
“Kuna ukamataji mwingi wa vyombo, ukipita kituo cha polisi utakuta pikipiki nyingi zimepangwa, utajiuliza kwanini hizi pikipiki haziondoki pale, kwa sababu kama ni ushahidi wa makosa yasikilizwe ahukumiwe na kazi iendelee.
“Lakini, vyombo vinabaki pale muda na muda… Utadhani wenyewe wamevitelekeza, nadhani iangaliwe kwa undani kero hizi ndogo ndogo zinasababishwa na nini,” alisema.
Rais Samia alielekeza Jeshi hilo kujikita kutoa elimu kwa kutumia mitandao ya kijamii kwani kundi kubwa la vijana kwa sasa limejielekeza huko.
Aidha, alilitaka kuwekeza katika shughuli za utafiti ili kupata suluhu ya kisayansi na kimfumo ya namna ya kupunguza ajali za barabarani kwa kushirikiana na vyuo vya usafirishaji na ufundi.
Alisema suala la usalama barabarani linapaswa kuwa ajenda ya kitaifa na kupewa uzito mkubwa kwa kuwa, linagusa kila kona na ajali hazichagui zimuondoe nani na zimuache nani.
Aliwataka wadau wa usalama barabarani, Wizara na mamlaka zote kushirikiana katika mapambano ya ajali za barabarani ili wawe na kauli moja.
Alilipongeza baraza kwa kufanya kazi kizalendo, akisema hawana bajeti au fungu linalowaendesha.

Hata hivyo, hakukubaliana na ombi lao la kutaka lipewe sehemu ya faini zinazotozwa kwa wanaotenda makosa katika usafirishaji ili kujiendesha, akisema itasababisha nguvu nyingi kutumika katika utozaji badala ya kudhibiti ajali.
“Ningependa kuona kwa kiasi kikubwa, makosa yanadhibitiwa barabarani na kuepuka hizo tozo badala ya kukimbilia utozaji,” alisema.
Aidha, Rais Samia alimwagiza IGP, Simon Sirro, kubadilisha teknolojia ya ukaguzi wa magari tofauti na inayotumika sasa ambayo huchukua muda mwingi kukagua magari machache.
“Ufanyaji wenyewe wa ukaguzi unachosha na umeshapitwa na wakati ni vyema sasa kutumia vifaa vya kisasa katika ukaguzi ili kukagua magari mengi zaidi na kukusanya fedha nyingi zaidi, napendekeza fedha za ‘strickers’ ndizo zitumike kuendesha baraza,” alisema.

Alilitaka Jeshi la Polisi kujadiliana na sekta binafsi juu ya kushirikiana katika ukaguzi wa magari ili kurahisisha hilo.
Katika hafla hiyo pia, Rais Samia alikabidhi Pikipiki 26 zilizotolewa na wadau wa bima kwa Jeshi la Polisi kusaidia utendaji kazi.