MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro, amemtaka Kamishna wa Polisi Zanzibar, Awadhi Juma Haji, kuhakikisha anakomesha vitendo vya kihalifu yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya na udhalilishaji visiwani humo.
IGP Sirro aliyasema hayo jijini Dodoma, wakati akimwapisha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Awadhi aliyepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na kuteuliwa na Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Samia Suluhu Hassan, kuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar.
“Zanzibar unaifahamu changamoto utakayokumbana nayo ni dawa za kulevya, udhalilishaji, makosa yenye viashiria vya ugaidi, ajali na rushwa nenda katende kazi,” amesema.
Alimwelezea Kamishna Awadhi kwamba ni mzoefu katika Jeshi hilo hususan visiwani humo, kwa kuwa aliwahi kufanya kazi katika maeneo kadhaa.
Kwa upande wake, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Awadhi alimhakikishia IGP Sirro kuwa, atafanyia kazi maelekezo yote na kuhakikisha visiwa hivyo vinatawaliwa na amani.
“Nakushukuru afande kwa sababu umenipa nafasi mbalimbali ambazo zimetoa dira hadi nimeonekana na nakuahidi yote uliyoniambia nitatekeleza kwa nchi yangu,” alisema.
Naye aliyekuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kamishna wa Polisi Mohammed Haji Hassan, alisema kazi ya Jeshi hilo ni kulinda usalama na heshima ya nchi, hivyo Kamishna Awadhi atakwenda kuendelea pale alipoishia yeye.
NA MWANDISHI WETU