MTAKWIMU Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa, amesema maandalizi ya sensa ya watu na makazi, yamefika asilimia 50 na sasa wanaendelea na utengaji wa maeneo ya kuhesabu watu.
Kauli hiyo ameitoa katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dar es Salaam, alipokuwa akipokea msaada wa kompyuta 20 na kompyuta mpakato 28 zilizotolewa kwa ofisi hiyo na Serikali ya Uingereza, ili kuchakata takwimu.
Dk. Albina amesema mbali na kutenga maeneo ya kuhesabu watu, kazi zingine wanazozifanya ni kuhamasisha wananchi kushiriki katika sensa.
Ameongeza kuwa, serikali inatarajia kufanya sensa ya TEHAMA, hivyo wanahitaji kompyuta 40 na zilizopo ni 20.
Naye, Mwakilishi wa Ofisi ya Mambo ya Nje na Maendeleo, Jumuiya ya Madola Maendeleo, Kemi Williams, alisema anatambua umuhimu wa sensa kwa kila nchi, kutokana na ukaribu ndiyo maana wameamua kuunga mkono.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anne Makinda, amesema sensa ni kitu muhimu, si hiari hivyo kila mtu anapaswa alione ni jambo la maendeleo.
Alisema serikali inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa shule, vituo vya afya, hivyo sensa ni muhimu kwa maendeleo na huleta umoja.
Aidha, alisisitiza kwamba, serikali imejidhatiti kufanya sensa kwa njia ya TEHAMA, hivyo inahitaji ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali.
Alisema serikali ya Uingereza, imetoa msaada huo kwa kutambua dunia ni moja na takwimu zitakazopatikana zitasaidia kuitambua sura halisi ya nchi.