KATIKA kuboresha huduma ya usafiri wa reli nchini, serikali imetia saini mkataba wa ununuzi wa mabehewa 22 ya abiria na vipuri vya ukarabati wa mabehewa 37 ya abiria.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Fred Mwakibete, aliyasema hayo Bungeni, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Emmanuel Mwakasaka.
Mbunge huyo alitaka kujua mikakati ya serikali katika kuboresha mifumo ya upatikanaji wa tiketi kwa wasafiri wa reli ya kati.
Akijibu swali hilo, Mwakibete alisema kwa sasa serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha na imeanza matumizi ya mifumo ya kielektroniki kwa maeneo yote yenye huduma ya intaneti ikiwemo Tabora ili kuboresha huduma na kurahisisha upatikanaji wa tiketi mtandao kwa wananchi.
Aliongeza kuwa mfumo wa ukatishaji tiketi wa kieletroniki ulizinduliwa Aprili, mwaka huu kwa lengo la kupunguza matumizi, kuongeza mapato na ufanisi wa shirika na kuondoa mianya ya upotevu wa mapato.
Aidha, alieleza kuwa serikali inaendelea na jitihada za kuongeza vitendea kazi ambavyo ni injini na mabehewa kwa lengo la kuboresha huduma kwa kuhudumia wananchi wengi zaidi na tayari imetia saini mkataba wa ununuzi wa mabehewa 22 ya abiria na vipuri vya ukarabati wa mabehewa 37 ya abiria.
Naibu Waziri huyo alisema kuongezeka kwa vitendea kazi hivyo kutaongeza idadi ya safari za treni za abiria, hivyo kupunguza changamoto ya upatikanaji wa tiketi kwa wakati.