UMOJA wa Machifu Tanzania (UMT), umetaja siri ya kilichowasukuma kumsimika Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa Mkuu wa Machifu wote nchini, kwamba inatokana na imani kubwa waliyonayo juu ya kiongozi huyo mkuu wa nchi.
Pia, wametaja uamuzi wa Rais Samia kurekodi filamu ya kutangaza vivutio vya utalii nchini ukiwemo utamaduni wa Mtanzania, ambao unabeba matarajio makubwa ya wananchi wa makundi mbalimbali, hivyo anapaswa kuungwa mkono.
Akizungumza na UhuruOnline, baada ya uzinduzi Tamasha la Utamaduni lililozinduliwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu wa UMT, Aron Mikomangwa Nyamilonda III, alisema imani yao kubwa kwa Rais Samia inatokana na uimara wake anaoendelea kuuonyesha tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania.
“Anastahili heshima hiyo kwa taifa, ndiye Rais wa nchi, ni haki yake, hata mila zetu hazizuii mwanamke kuwa Chifu, ukiangalia Uingereza wao wana Malkia, hivyo Rais Samia ndiye Malkia wetu na tumempa heshima hiyo ili kurejesha maadili na kulinda mila na desturi zetu kuhakikisha hazipotei,” alisema.
Chifu Nyamilonda III, alisema kumsimika Rais Samia kuwa kiongozi mkuu wa Machifu, pia kumechochewa na ukweli kuwa ndiye Amiri Jeshi Mkuu.
Kwa upande wake, Chifu Sisco Ng’enyi wa Singida, alifichua siri kuwa mchakato wa kumsimika Rais Samia kuwa Chifu wa Machifu wote nchini, haukuanza jana, bali ulianza siku nyingi lakini ulichelewa baada ya kuingiliana na kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
“Ilikuwa tumsimike Hayati Magufuli kuwa chifu wetu, kwa bahati mbaya haikuwezekana ndipo tukajielekeza kwa Rais Samia baada ya kuona mwelekeo wake; na ni pale tulipobaini kuwa nchi yetu inaelekea kupoteza utamaduni wake na kutumbukia katika mila za kigeni,” alisema Chifu Ng’eni.
Alisema tayari wameandika andiko la kuhusisha utamaduni, mila, desturi na maadili, hivyo Rais Samia akiwa Mkuu wa Machifu na msimamizi mkuu wa sheria za nchi, atawasaidia kusimamia hilo.
Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Kigoma, Alfred Kimenyi, alisema ushiriki wao katika mambo mengi ya mila na ujenzi wa taifa kimaadili, kiuchumi na kijamii, utaifanya Tanzania kuwa taifa bora chini ya Rais Samia na kwamba, hizo ni miongoni mwa sababu za kumsimika kuwa Chifu Mkuu wa Machifu.
“Kuamua kurekodi filamu ya vivutio vya rasilimali za madini, utamaduni wetu, kutaokoa mila zetu na maadili yetu yasipotee, pia ni matarajio yetu Machifu, Watanzania watanufaika kiuchumi na kijamii kupitia maono ya Rais Samia,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Msagasa Fundikira, aliitaja sababu nyingine ya kumsimika Rais kuwa chifu ni kupenda na kuthamini kwake mila.
“Nchi yetu mila na maadili yameporomoka sana, yeye ameamua kuweka mbele kuhakikisha mila hazipotei, hivyo kumpa wadhifa huo hatuna mashaka naye ili atuinue. Tunamuunga mkono, tuna vyanzo na vivutio vingi vya utalii ila tulikuwa hatujazinduka vizuri,” alisema.
MABULA
Akifungua tamasha hilo, Dk. Angeline alisema serikali ya awamu ya sita imedhamiria kutangaza mila na desturi, kuzilinda na kuzihifadhi kwa ajili ya urithi wa vizazi vijavyo.
Pia, alisema serikali inatambua jitihada zinazofanywa na Machifu kulinda, kudumisha mila, kurithi na kuthamini utamaduni; ukiwemo wa Makumbusho ya Utamaduni wa Kabila la Wasukuma (Bujora).
“Rais Samia kuamua kutengeneza filamu sasa utamaduni wa Mtanzania unakwenda kuanikwa hadharani; na dunia itatambua tuna mila na desturi zetu, maana baada ya miaka mingi jamii bado inatambua na kuzithamini mila hizo na kuzienzi,” alisema.
Na BALTAZAR MASHAKA, Magu