SERIKALI mkoani Dar es Salaam, imewaongeza siku 12 wafanyabiashara ndogo ‘wamachinga’ ambazo zitamalizika Oktoba 30, mwaka huu, kuondoka rasmi katika eneo la Kariakoo.
Siku hizo zimeongezwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, alipokuwa akiwahutubia wafanyabiashara hao katika eneo la Kariakoo.
Amesema leo Oktoba 18, 2021, imetimia rasmi siku 30 zilizotolewa kwa wamachinga kuondoka katika maeneo yasiyo rasmi na kwenda sehemu walizopangiwa kama ilivyoelekezwa na serikali.
“Ninawapa hadi tarehe 30, mwaka huu muwe mmeondoka kwa hiyari. Ninamuomba radhi Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), kwa sababu sikumshirikisha na kumuomba kuongeza hizi siku 12,” amesema Makala.
Amesema siku hizo 12 ametoa ili wafanyabiashara hao wajipange vizuri na kuondoka kwa hiyari katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Amesema baada ya siku hizo kumalizika ni marufuku wamachinga kufanyabiashara yoyote mbele ya maduka au kukinga maduka hayo katika eneo la Kariakoo.
MANEO HAYA NI MARUFUKU
Pia ametaja maeneo matano ambayo wamachinga watatakiwa kuondoka katika mkoa wa Dar es Salaam, ambayo ni waliojenga juu ya mifereji, mitaro, hifadhi za barabara, shule, vyuo, taasisi za serikali, njia za watembea kwa miguu na nje ya maduka.
“Nilifanya uchungizi hapa. Kuna machinga wenye vitambulisho wanafanya biashara ya bidhaa za jumla. Hii inasababisha upotevu mkubwa wa mapato hapa Kariakoo,” amesema.
Amesema pia wapo wachache wamejimilikisha maeneo ya Kariakoo ambapo huwauzia maeneo na meza wamachinga kwa gharama ya sh. milioni mbili hadi tatu kwa meza moja.
“Kuna mtu aliweka meza mbele ya duka. Ilibidi mwenye duka kununua meza hizo kwa sh. milioni 20. Yaani meza moja kwa sh. milioni 10 ili meza hizo ziondoke mbele ya duka lake,” amesema.
RIPOTI YA KUONDOKA WAMACHINGA
Makala amesema tangu utekelezaji wa kuwapanga upya wamachinga uanze mkoani humo, kumekuwa na mwitikio mkubwa na kuupongeza uongozi wa wafanyabiashara kwa usimamizi.
“Katika maeneo mengi wamachinga ambao walikuwa katika maeneo yasiyo rasmi wanaondoka kwa hiyari yao na usimamizi wa uongozi wao. Ninashangaa hapa Kariakoo bado,” alisema.
Amesema hali ya usalama, hatari ya kutokea kwa ajali barabarani na uchafuzi wa mazingira vimekithiri Kariakoo ambapo kwa upande wa usalama ameagiza operesheni nzito kusaka wahalifu ifanyike.
Makala amesema mikakati mingine ya kusaidia wamachinga mbali na kuwapeleka katika masoko ya kisasa, wanafanya tathimini ya kuugeuza ukumbi wa Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam (DDC), uliopo Kariakoo utumiwe na wafanyabiashara.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamachinga Kariakoo (KAWASO), Steven Lusinde, alipongeza hatua hiyo ya serikali ya kuwapanga upya na kuwasisitiza wenzake kuondoka kwa hiyari.
Na CHRISTOPHER LISSA