WAMACHINGA wa Kata ya Kigamboni, Dar es Salaam, wamekipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kutoa tamko la kuwalinda wakati operesheni ya kuhamishiwa katika maeneo mengine ya kufanyia biashara.
Wakizungumza na waandishi wa habari, Kigamboni, Dar es Salaam, walisema wamepata tumaini jipya baada ya tamko lililotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, kuhusu utaratibu wa kupangwa.
Mwenyekiti wa Machinga, Wilaya ya Kigamboni, Mengi Kajato, alisema lengo la Rais Samia Suluhu Hassan ni zuri, lakini linaharibiwa watendaji katika utekelezaji wake.
“Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan na anafanya kazi kubwa sana, lakini linapokuja suala la utekelezaji kuna kuwa na sintofahamu, sisi wafanyabiashara tunahitaji kuendelea kufanya biashara, pia hatujakataa kupangwa ila utaratibu wake siyo mzuri,” alisema.
Kwa mujibu wa Kajato wamekuwa waathirika katika mchakato wa kuwapanga kwa kuwa wapo waliopoteza mali zao na mabanda ya kufanyia biashara kuvunjwa bila ya kufuata utaratibu.
“Wamachinga siyo wakorofi na wanaichukulia kazi hiyo kama ajira yao, lakini baadhi ya viongozi wanakwenda kinyume na agizo lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hasasan,” alisema.
Kajato alisema maeneo waliyoambiwa waende kufanyia biashara ni Pombe shop, Stoo ya mkaa na kwa Mzee Kisiki, ambayo siyo rafiki kwa kuwa hakuna huduma muhimu za kijamii kama vile maji, vyoo, barabara na hakufikiki kirahisi.
Katibu wa CCM, Tawi la Raha Leo, Joha Baton, alisema vibanda vyao vimeondolewa kwa kupewa taarifa ghafla ya kuwataka kuondoka na usiku wa saa saba walifika watu ambao walivivunja na kusababisha upotevu wa mali zao.
“Hatujaitwa katika kikao wala kushirikishwa kwa jambo lolote, yaani hatuji chochote kinachoendelea hadi hivi sasa. Rais wetu hakuagiza hiki kinachofanyika sasa hivi la kutupanga machinga,” alisema.
Mama lishe Farida Msofe, aliwaomba viongozi wa wilaya hiyo kukaa kikao cha pamoja na wafanyabiashara hao ili kuweka utaratibi mzuri wa kuwapanga kuliko kuwabomolea vibanda vyao na kusababisha mali zao kupotea.
Hata hivyo, Farida alisema faraja waliyoipata kwa Chama Cha Mapinduzi, kwa kutambua mchango wa wamachinga hatimaye kutoa tamko la watendaji kutowanyanyasa wamachinga.
Na JUMANNE GUDE