SERIKALI imeyataja mafanikio 10 yaliyopatikana katika sekta ya kilimo yaliyojikita kuimarisha huduma za ugani, ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, uhifadhi wa mazao na upatikanaji masoko ya mazao ya kilimo.
Imesema imejidhatiti kuliwezesha taifa kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula na kuuza nje ya nchi na kufanya mwelekeo wa uzalishaji wa mazao ya chakula kuwa wa kibiashara.
Waziri wa Wizara ya Kilimo, Hussein Bashe, aliyataja mafanikio hayo, alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2022/2023, Bungeni jijini Dodoma.
Bashe alisema ili kufikia lengo la ukuaji wa sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, bajeti ya mwaka 2022/2023 ni msingi muhimu kufikia lengo kuu hilo.
MAFANIKIO YALIYOPATIKANA
Waziri Bashe alisema Rais Samia Suluhu Hassan, ameongeza bajeti ya utafiti wa kilimo kutoka sh. bilioni 7.35 hadi sh. bilioni 11.63, huduma za ugani kutoka sh. milioni 603 hadi sh. bilioni 11.5, umwagiliaji kutoka sh. bilioni 17.7 hadi sh. bilioni 51.48 na uzalishaji wa mbegu kutoka sh. bilioni 5.42 hadi kufikia sh. bilioni 10.58
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Sita, imeongeza fedha za ununuzi wa nafaka kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) kutoka sh. bilioni 19 mwaka 2020/2021 hadi sh. bilioni 119 mwaka 2021/2022.
“Hadi Aprili mwaka huu, fedha hizo zimewezesha ununuzi wa tani 183,045.384 za mahindi, mpunga na mtama. Hatua hiyo, itaiwezesha nchi kuwa na uhakika wa chakula na kuuza katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Katika kipindi hicho, serikali imewezesha ununuzi wa pikipiki 7,000 kwa ajili ya maofisa ugani ili kurahisisha usafiri, vishikwambi 384 kwa maofisa ugani 384, visanduku vya ufundi 6,700 kwa maofisa ugani na vifaa vya kupima afya ya udongo kwa ajili ya kupima udongo kwa halmashauri 143. Jumla ya sh. bilioni 9.2 zimetumika kununua vifaa hivyo,”alisema.
Pia, alisema linalomwagiliwa limeongezeka kutoka hekta 695,045 mwaka 2020/2021 hadi hekta 727,280.6 mwaka 2021/2022, sawa na asilimia 60.6 ya lengo la hekta 1,200,000 ifikapo mwaka 2025 kama inavyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.
Alisema katika kipindi hicho, vyama vya umwagiliaji vilivyosajiliwa chini Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji Namba. 4 ya Mwaka 2013 na Kanuni zake za mwaka 2015, vimeongezeka kutoka 180 mwaka 2020/2021 hadi vyama 312 mwaka 2021/2022.
Kadhalika, alisema serikali imesimamia dhana ya kilimo ni biashara kwa kuimarisha mahusiano ya kimataifa ambayo yamefungua fursa ya masoko ya mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi.
“Jitihada hizo zimewezesha kupatikana kwa fursa za masoko mapya ya mazao nje ya nchi ikiwemo soko la parachichi katika nchi za India na Afrika Kusini, ndizi nchini Kenya na mchele nchini ubelgiji baada ya kukidhi viwango vya ubora.
“Upatikanaji wa masoko umeongeza mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi ambapo mauzo ya mchele yameongezeka kutoka tani 184,521 zenye thamani ya sh. bilioni 176.4 mwaka 2020 hadi tani 441,908 mwaka 2021 zenye thamani ya sh. bilioni 476.8 mwaka 2021 na mahindi kutoka tani 92,825 zenye thamani ya sh. bilioni 58 mwaka 2020 hadi tani 189,277 zenye thamani ya sh. bilioni 72.4 mwaka 2021,” alibainisha.
Kwa upande wa parachichi alisema mauzo ya zao hilo yameongezeka kutoka tani 6,702 zenye thamani ya sh. bilioni 14.9 mwaka 2020 hadi tani 12,250 zenye thamani ya sh. bilioni 24.9 mwaka 2021.
Bashe alisema serikali imeongeza mtaji wa Benki ya Kilimo (TADB) kutoka sh. bilioni 60 mwaka 2021 hadi sh. bilioni 268 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 346.7.
“Ongezeko hilo limewezesha TADB kutoa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 116.63 kwenye miradi 197 ya maendeleo na kufanya jumla ya mikopo iliyotolewa tangu benki hiyo ianzishwe kufikia sh. bilioni 482.4,” alisisitiza.
Aidha, alieleza kuwa benki hiyo imewezesha wakulima 1,527,175 kupata dhamana ya mikopo ya kiasi cha sh. bilioni 144 huku serikali ikiziwezesha benki za biashara kupunguza riba za mikopo ya kilimo kutoka kati ya asilimia 17 na 20 hadi kufikia asilimia tisa.
Alisisitiza kuwa hatua hiyo imewezesha wakulima kupata pembejeo kwa wakati, kufufua na kuanzisha viwanda vidogo vya kuongeza thamani.
Vilevile, alieleza kuwa Serikali ya Rais Samia imefanikisha uuzaji wa soya nje ya nchi kufikia tani 53,594.35 mwaka 2020/2021 ikilinganishwa na tani 2,647 mwaka 2019/2020 ambapo kampuni 80 za Kitanzania zimesajiliwa kuuza soya nchini China.
Pia, alisema Serikali kupitia CPB imefungua vituo vya mauzo katika miji ya Juba (Sudan Kusini) na Lubumbashi (DR Congo) na kukodi maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 na 2,000 mtawalia.
“Serikali imetoa ruzuku za pembejeo za kilimo kwa mazao ya korosho, tumbaku na pamba zenye thamani ya sh. bilioni 178.8. Katika kipindi hicho serikali imewezesha uundaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika na ununuzi wa magari 15, pikipiki 137 na kompyuta 82 kwa ajili ya kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika nchini,” alisisitiza.
MAFANIKIO ZIARA ZA RAIS SAMIA
Akizungumzia mafanikio ya ziara ya Rais Samia katika nchi mbalimbali, Bashe alisema nchini Ufaransa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imesaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya sh. bilioni 210 wenye lengo la kuimarisha benki hiyo kutoa mikopo ya muda mfupi na mrefu kwa sekta ya kilimo nchini.
Katika uwekezaji kwenye sekta ya mbolea, alisema kwa sasa kiwanda cha Itracom Fertilizer Limited kutoka Burundi, kinajenga kiwanda kikubwa cha mbolea Jiji la Dodoma chenye thamani ya dola milioni 180 ambapo kinatarajiwa kutoa ajira za kudumu kwa wafanyakazi 3,000 na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mbolea tani 600,000 kwa mwaka.
Aidha, jitihada kubwa za kufungua masoko kwa ajili ya mazao ya kilimo ambayo awali ilikuwa changamoto kubwa, kutokana na juhudi za Rais Samia kuimarisha mahusiano na mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kumechochea upatikanaji wa masoko ya mazao mbalimbali.
Alisema mauzo ya maharage kutoka Tanzania kwenda Jumuiya ya Afrika Mashariki yameongezeka na kufikia dola milioni 193 pamoja na uondoaji vikwazo 56 vya biashara kati ya 64 vilivyokuwepo kati ya nchi ya Tanzania na Kenya.
“Jitihada hizo zimepelekea ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Kenya kufikia dola milioni 905. Upatikanaji wa soko la China kwa ajili ya mazao ya maharage ya soya na muhogo, jambo ambalo limetoa fursa ya soko la uhakika kwa wakulima wa mazao hayo nchini,” alisisitiza.
Katika kutekeleza majukumu ya wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2022/2023, Bashe aliliomba Bunge liidhinishe sh. bilioni 751.1 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za kawaida na miradi ya maendeleo.
NA MUSSA YUSUPH, DODOMA