KATIKA kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika, serikali imepanga kutekeleza miradi ya maji kutoka vyanzo vya uhakika vikiwemo Ziwa Tanganyika, Nyasa, Victoria na mito mikubwa ya Ruvuma, Rufiji, Kiwila, Songwe na Kagera.
Akitoa taarifa ya mafanikio ya Wizara ya Maji, katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Waziri wa Maji Jumaa Aweso, alisema kumekuwa na maendeleo makubwa katika sekta hiyo.
“Katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara wastani wa wakazi wanaopata huduma ya maji safi na salama, umeongezeka kutoka asilimia 25 ya wakazi wote wanaoishi mijini mwaka 1961, hadi kufikia wastani wa asilimia 86 mwaka 2021,” alisema Aweso.
Alisema miradi hiyo itahusisha ujenzi wa mitandao ya kusafirisha maji kutoka maeneo yenye maji mengi na kuyapeleka yale yenye uhaba.
Katika kusimamia rasilimali za maji, alisema serikali imeanzisha bodi za maji za mabonde tisa zikiwa na kazi ya kusimamia, kuendeleza, utayarishaji wa mipango ya uwiano wa matumizi mbalimbali ya maji na kufanya utafiti wa maji.
“Nchi yetu ina rasilimali za maji zipatazo mita za ujazo bilioni 126 ambapo lita bilioni 105 ni maji juu ya ardhi na lita bilioni 21 chini ya ardhi,” alisema.
Kuhusu huduma za maji vijijini, alieleza hadi Juni, mwaka huu miradi 566 kati ya 632, sawa na asilimia 89.6 imekamilika.
Pia alisema miradi 115 kati ya 177, sawa na asilimia 65, imeanza kutoa huduma kwa wananchi na miradi yote iliyosalia itakamilishwa ifikapo Juni, mwakani.
Aidha, alisema hadi Juni, mwaka huu miradi mipya 912 ya maji vijijini ilianzishwa ambapo 458 imekamilika na kuanza kutoa huduma.
“Kukamilika kwa miradi hiyo na kuanza kutoa huduma kumeongeza wastani wa upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kutoka asilimia 64.8 mwaka 2019 hadi asilimia 72.3 kufikia Juni, mwaka huu.
Aliongeza kuwa: “Hadi sasa, jumla ya vijiji 8,708 kati ya 12,327 vinapata huduma ya maji safi na salama na hivi sasa, kuna vyombo vya utoaji wa huduma ya maji vijijini 2,115 ambavyo vimeajiri wahasibu 1,362 na mafundi 1,611.”

Kwa upande wa ufundi, alisema RUWASA ipo katika mchakato wa kuanzisha vituo maalumu vya utoaji wa msaada wa kiufundi katika ngazi ya mkoa, ambavyo vitakuwa na wajibu wa kusaidia Jumuiya za watoa huduma vijijini.
Pia alisema wizara kupitia RUWASA ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha utaratibu mpya wa makusanyo ya mauzo ya maji vijijini, ambapo mauzo yote yatapitia mfumo wa makusanyo serikalini (GePG).
Kuhusu huduma ya maji mijini inayotolewa na Mamlaka za Maji ambazo zilianzishwa kwa Sheria ya Maji Mijini ya mwaka 1997, alieleza kuwa lengo lilikuwa kuboresha huduma ya maji katika maeneo ya mijini ili kuendana na kasi ya maendeleo ya miji.
Alisema hadi Oktoba, mwaka huu, mamlaka 96 za miji mikuu ya mikoa, miji midogo na miradi ya kitaifa zimeanzishwa na zinatoa huduma ya maji.
MWELEKEO MAJI
Alisema katika kufikia malengo ya sekta, wizara inatekeleza mipango kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Malengo ya Maendeleo Endelevu 2016 – 2030, Awamu ya Tatu ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26) na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, alisema serikali imeendelea kutekeleza mipango mbalimbali ambayo imekusudia kufanikisha malengo ya Sekta ya Maji ikiwemo, kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio mijini inafikia zaidi asilimia 95 mwaka 2025 na vijijini inafikia asilimia 85 mwaka 2025.
Na FRED ALFRED, Dodoma