WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imefanya uamuzi wa kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi nchini ili wananchi hususan vijana wapate ujuzi na ufundi wa aina mbalimbali utakaowasaidia kujiajiri na kuajiriwa.
Kauli hiyo aliitoa baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa chuo cha ufundi stadi cha Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya.
Aliagiza ujenzi huo ukamilike kwa wakati ili malengo ya serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya ufundi chuoni hapo yanafikiwa.
Majaliwa alisema serikali imeamua kujenga vyuo hivyo vya ufundi stadi ili kufungua milango ya ajira kwa kuwa mafunzo yanayotolewa yatawawezesha wahusika kuajiriwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda.
“Ninawaomba wananchi muendelee kuwa na imani na serikali yenu,” alisema.
Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Mbeya uhakikishe katika eneo hilo la kijiji cha Mbugani kinapojengwa chuo hicho kunakuwa na huduma zote za kijamii zitakazotosheleza matumizi ya eneo hilo zikiwemo za maji safi na salama na umeme.
Waziri Mkuu alisema Rais Samia anawasihi wananchi waendelee kuyalinda maeneo yao yaendelee kuwa tulivu ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Suala la kuimarisha ulinzi na usalama ni jukumu la wananchi wote, hivyo tuendelee kushirikiana katika kuimarisha ulinzi,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dk. Pancras Bujulu, alisema mradi huo una majengo 17, ambayo ni la utawala, karakana nne, jengo la madarasa, mabweni mawili, bwalo la chakula, majengo matatu ya vyoo, nyumba ya mkuu wa chuo, nyumba ya familia mbili za watumishi, jengo la mitambo ya umeme, jengo la stoo na jengo la walinzi.
Dk. Bujulu alisema chuo hicho kitakapokamilika kinatarajiwa kuanza na fani sita za muda mrefu ambazo ni uhazili na kompyuta, ushonaji na ubunifu wa mitindo, uashi, umeme wa majumbani, ufundi magari na uchomeleaji na uungaji wa vyuma.
Alibainisha kuwa gharama za ujenzi wa chuo hicho ni sh. bilioni 1.6.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Majaliwa alikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya – Makongorosi yenye urefu wa kilometa 39 unaotarajiwa kukamilika Februari 27, mwakani.
Mradi huo unaogharimu sh.bilioni 67.2 umegharamiwa na serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.
Baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara hiyo unaotekelezwa na Mkandarasi China Railway 15 Bureau Group Corporation, uliofikia asilimia 98, Majaliwa alitoa wito kwa wakazi wanaoishi katika maeneo inapopita barabara hiyo watumie fursa ya ujenzi huo kwa kuanzisha miradi itakayowaongezea tija.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Mbeya Mhandisi Eliazary Rweikiza, alisema mradi huo ulianza kutekelezwa Oktoba 30, 2017 kwa muda wa mkataba wa miezi 46 ambapo ulitarajiwa kumalizika Agosti 31, mwaka huu.
Hata hivyo, alisema serikali imeongeza mkataba wa ujenzi wa mizani ya kupimia magari inayojengwa katika kijiji cha Matundasi ili kulinda barabara hiyo, hivyo kuufanya mradi huo kukamilika Februari 27, mwakani.
NA MWANDISHI WETU