WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali inaangalia utaratibu utakaofaa kuhusu suala la uhifadhi katika eneo la Loliondo lililopo katika Wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha.
Ametoa kauli hiyo Februari 14, 2022, wakati akizungumza na wadau wa uhifadhi katika kikao kilichofanyika Wasso-Loliondo ambapo alisema serikali imepokea maoni waliyoyatoa, yatayojumuishwa na kuyawasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Katika mjadala wetu wa leo (jana), mmetoa maoni nasi tumeyapokea. Bado serikali inayaangalia maslahi mapana ya umma. Tutawashirikisha pia ni lipi lina maslahi mapana kwa Watanzania,” alisema.
Majaliwa alisema alichokwenda kufanya ni utekelezaji wa ushauri uliotolewa na wabunge kwa serikali kupitia Mwenyekiti wa Kamati wa Maliasili na Utalii, iliyoielekeza serikali iende katika maeneo ya Loliondo, Ngorongoro na Sale na kuzungumza na wananchi.
“Kama ambavyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza lazima tuimarishe utalii na kuhakikisha wananchi wanashirikishwa, waheshimiwa wabunge ambao ndio wawakilishi, wametoa maoni yao ikiwemo kushauri suala la ushirikishwaji na ndiyo maana leo (jana), nimekuja hapa kuwasikiliza,” alisema.
Waziri Mkuu alisema kuwa, kila mmoja anatambua idadi ya watu na mifugo imeongezeka ndani ya hifadhi na kwamba, pasipotafutwa suluhisho la kudumu, hifadhi zitaathirika. “Sisi sote tunatambua eneo hili ni la utalii, lazima tufike mahali tuamue kama tunataka utalii au la,” alisema.
Amesema amefarijika kusikia kwamba, wachangiaji wote waliozungumza hakuna aliyesema ardhi ni yao.
“Kati ya mambo yamenifariji, sijasikia mtu akisema ardhi yetu, ardhi yetu. Sote tunatambua kuwa ardhi iliyo ndani ya mipaka ya nchi hii ni ya umma, lakini tumeikasimu kwa Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Katika kikao hicho, wananchi wa makundi mbalimbali, walipewa nafasi kutoa maoni yao akiwemo mbunge, madiwani, malaigwanan, wanamije (batemi) na wenyeviti wa vijiji.
Katika maoni yao, wengi wao walisema wako tayari kushirikiana na serikali kuendelea kutunza rasilimali za taifa.
Waliomba wapatiwe elimu ya uzazi wa mpango, wapimiwe ardhi za vijiji ili kupunguza migogoro inayojitokeza mara kwa mara. Wilaya ya Ngorongoro ina tarafa tatu za Loliondo, Sale na Ngorongoro.
Na WAANDISHI WETU, Ngorongoro