WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinachangia katika kuinua uchumi wa Watanzania.
Aliyasema hayo, baada ya kuzindua Maonyesho ya Nne ya Teknolojia na Uwekezaji katika sekta ya madini mkoani Geita, kuwa maonyesho hayo yamekuwa na manufaa makubwa katika kuhamasisha wananchi kujihusisha na shughuli za madini.
Alisema serikali ya awamu ya sita, itaendelea kufanya marekebisho ya baadhi ya kanuni na taratibu zinazosimamia uchimbaji na biashara ya madini, kwa lengo la kuwezesha wananchi na wadau wengine kushiriki ipasavyo katika uchumi wa madini na kuongeza uwekezaji.
Hata hivyo, Majaliwa aliwataka wadau wa sekta ya madini nchini wazingatie na wafuate sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia sekta hiyo, ili kuondoa usumbufu na kurahisisha utendaji wa shughuli zao na serikali, kwa manufaa ya pande zote.
Alisema sekta ya madini imeendelea kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa taifa na maendeleo ya mtu mmoja mmoja nchini.
“Matarajio ya serikali ni kuongeza zaidi mchango huo kupitia shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, usafishaji madini, usanifu madini na utoaji wa huduma katika shuguli za madini.
“Lengo la serikali ni kufungamanisha ustawi wa sekta ya madini kwa kuwezesha wananchi na wadau mbalimbali kushiriki ipasavyo katika uchumi wa madini na kuongeza uwekezaji, ili kukuza sekta nyingine za kiuchumi na huduma zikiwemo viwanda, ujenzi, usafirishaji, mawasiliano na nishati.
Waziri Mkuu alisema serikali
imeendelea kuweka mikakati ya kuimarisha Taasisi ya Jiolojia Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ili zitoe huduma bora na nafuu kwa wachimbaji wadogo pamoja na uchorongaji wa miamba kwa lengo la kujua uwepo na wingi wa mashapo.
Alisema hatua hiyo itasaidia wachimbaji wadogo kuendesha shughuli zao kwa tija na uhakika, hivyo kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
“Natoa wito kwa wachimbaji kutumia taasisi hizi ili muweze kupata taarifa za mashapo ya madini na kuchimba kwa uhakika.
“Katika hili, ninaielekeza Wizara ya Madini ihakikishe suala la Local Content (kipengele cha ushirikishwaji wa wazawa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati), linasimamiwa kikamilifu. Makampuni yote makubwa yatumie huduma za GST na STAMICO isipokuwa pale ambapo itathibitika wameshindwa ndipo waagize nje,” aliagiza.
Majaliwa alisema serikali itaendelea kuimarisha sekta ya madini nchini, ili kuiwezesha kufikia lengo la kuchangia asilimia 10 ya pato la taifa ifikapo mwaka 2025. “Ni ukweli usiopingika kwamba suala hili litafanikiwa endapo wadau wote tutashirikiana kuanzia hatua ya utafutaji, hadi biashara ya madini.”
Alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa vijana, wanawake na Watanzania wote kwa ujumla, kuchangamkia fursa zilizopo na zitakazojitokeza katika maeneo mbalimbali ya miradi ya madini nchini, ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi.
“Nyote mtakubaliana nami kuwa kuna miradi mingine mikubwa inatazamiwa kuanza hivi karibuni ukiwemo mradi wa Nyanzaga Mining uliopo Wilaya jirani ya Sengerema na mgodi wa madini ya Rare Earth Element uliopo Songwe. Kwa hiyo, jipangeni vizuri na mchangamkie fursa hizo.”
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, serikali katika mwaka 2021/2022 imefuta tozo ya Ongezeko la Thamani (VAT), kwa madini kutoka nje ya nchi yatakayouzwa katika masoko au kusafishwa nchini, kwa lengo la kuimarisha biashara baina ya nchi yetu na nyingine.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wafanyabiashara na wachimbaji wa madini kote duniani, waje kwa wingi kusafisha, kuuza na kununua madini katika masoko ya Tanzania yaliyotapakaa nchi nzima.
“Najua hata ninyi wachimbaji wetu hapa baadhi yenu mna migodi nchi jirani, basi leteni madini yenu hapa muuze kwa uwazi na uhakika kwenye masoko yetu,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Dotto Biteko, alisema Wizara ya Madini itaendelea kusimamia biashara ya madini nchini ili kuhakikisha ndoto ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuona Tanzania inakuwa kitovu cha biashara ya madini, inatimia.
Rais wa Muungano wa Wachimbaji Wadogo Tanzania, John Mbina aliipongeza serikali kwa namna inavyosimamia ukuaji wa sekta ya madini nchini.
“Wachimbaji wadogo wameendelea kuleta mapinduzi ya kikodi, mwaka jana walichangia sh. bilioni 180, hii ni ishara kwamba siku moja wachimbaji wadogo watasogea na kuwa wachimbaji wakubwa”
Awali, Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kusafisha madini ya dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR) kinachomilikiwa na Mtanzania, kilichopo eneo la Bombambili ambapo alisema kuwa serikali itafanya jitihada ili kuhakikisha kiwanda hicho kinafanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Waziri Mkuu aliyasema hayo baada ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa GGR, Sarah Masasi kuiomba serikali isaidie ili kiwanda hicho kinachotumia teknolojia ya kisasa kiweze kufanya kazi. Gharama ya ujenzi na ununuzi wa mitambo ya kiwanda hicho ni sh. bilioni 28.
NA MUANDISHI WETU