WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya ujenzi wa majengo ya ofisi na makazi kwa watumishi wa umma kwa lengo la kupunguza gharama za kodi ya pango na kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa watumishi nchini.
Katika kutimiza azma hiyo, amesema serikali itaendelea kuuboresha Mji wa Dodoma kwa kujenga miundombinu ya barabara, maji pamoja na nyumba za watumishi.
Waziri Mkuu aliyasema hayo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba 1,000 za makazi zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), katika eneo la Chamwino na Iyumbu, mkoani Dodoma.
“Hivi karibuni Rais Samia ametoa sh. bilioni 20 ambazo ni mkopo nafuu kwa Shirika la Nyumba la Taifa ili ziwe mtaji wa kujenga nyumba 1,000 katika maeneo ya Chamwino na Iyumbu jijini Dodoma ambao hadi kukamilika kwake, mradi huo utagharimu sh. bilioni 71 huku awamu ya kwanza ikitumia sh. bilioni 21.4 kukamilisha nyumba 404,” alieleza.
Majaliwa aliiagiza NHC kukaa pamoja na DUWASA, TARURA na TANESCO kuona namna bora ya kushirikiana na kufanikisha upatikanaji wa miundombinu hiyo muhimu ili kupunguza mzigo wa gharama kwa shirika hilo.
“Wakurugenzi wa Halmashauri hususan halmashauri mpya, tumieni Shirika la Nyumba la Taifa pamoja na Watumishi Housing ili kuharakisha ujenzi wa nyumba bora za watumishi wa Halmashauri kwa gharama nafuu,” alisema.

Kadhalika, aliliagiza shirika hilo kupunguza gharama za ununuzi kwa kununua vifaa yakiwemo mabati, mabomba, vigae kutoka kwa wazarishaji wa ndani ya nchi kwa kuweka oda maalumu ili miradi ikamilike kwa muda uliopangwa na kuhakikisha sheria na utaratibiu wa ununuzi unafuatwa.
Awali, akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa nyumba 100 katika eneo la Chamwino, Waziri Mkuu aliipongeza Wizara ya Ardhi pamoja na NHC kwa hatua ya ujenzi nyumba hizo pamoja na mpango wa ujenzi wa nyumba za makazi.
Majaliwa aliwapongeza wafanyakazi wakitanzania walioshiriki katika ujenzi wa nyumba hizo, ukiwa utekelezaji wa msisitizo wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikishwaji wa Watanzania katika ujenzi wa miradi mikubwa ya ujenzi.

Kwa Upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema serikali kupitia NHC haitaruhusu utaratibu wa mtu mmoja kununua nyumba nyingi katika eneo hilo na kisha kuanza utaratibu wa kupangisha, ila watatoa fursa sawa kwa Watanzania wa kada zote wanufaike na mradi huo.
Mkurugenzi wa NHC, Dk. Maulid Banyani, alisema awamu ya kwanza ya mradi wa nyumba 1,000 unaotekelezwa na shirika hilo mkoani Dodoma, ulianza Januari sita mwaka huu na kwa mradi wa Iyumbu na Chamwino ulianza Februari Mosi, mwaka huu.
“Mradi huu mkubwa unaohusisha ujenzi wa nyumba za makazi 1,000 katika Jiji la Dodoma utagharimu sh. bilioni 71 hadi kukamilika, ambapo awamu hii ya kwanza yenye nyumba 404 itagharimu sh. bilioni 21.4 na kazi kubwa ya ujenzi itakuwa imekalika ifikapo Desemba mwaka huu na kubakiwa na ukamilishaji wa kazi chache za nje ambazo nazo zitaisha Januari mwakani,” alibainisha.
Na MWANDISHI WETU, DODOMA