WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameziagiza taasisi zote zinazokusanya mapato nchini, kuhakikisha zinaweka mipango endelevu itakayoziwezesha kusimamia matumizi ya mapato hayo kwa manufaa Taifa.
Amesema serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kusimamia taasisi zote kuhakikisha zinakusanya mapato na kuweka mifumo imara ya kusimamia matumizi yake.
Majaliwa alitoa agizo hilo, baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Mbeya, mradi huo unajengwa katika Kata ya Iganzo jijini Mbeya unaogharimu Tsh. milioni 852.
Pia, Majaliwa alisema kwamba, serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha inaweka mipango madhubuti na usimamizi sahihi wa biashara na wafanyabiashara ili kunufaika na shughuli wanazofanya.
Aidha, Waziri Mkuu alitoa wito kwa uongozi wa CBE kuendelea kuweka mipango ya kuwafikia wanyabiashara wa ngazi zote na wale ambao hawajaanza kufanya biashara ili kuwatoa woga wa kuanzisha biashara.
“CBE endeleeni kuweka mpango mzuri wa kuwafikia na kuwapa elimu ya biashara wafanyabiashara wakubwa, kati na wadogo ili kuwawezesha kufahamu namna bora ya kuzifanya biashara zikue zaidi na kuongeza tija,”alisema.
Alisema katika kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya shughuli kwa ufanisi, serikali iliwaagiza viongozi wa serikali za mitaa kwa kushirikiana nao, watafute maeneo mazuri na kuyawekea miundombinu muhimu.
Naye Mkuu wa Chuo cha CBE, Profesa Emmanuel Mjema, alisema kuwa, mradi huo ulianza kutekelezwa Juni, mwaka huu na utakamilika Desemba, mwaka huu, chuo kimetoa Tsh. milioni 502 na Serikali Kuu, Tsh. milioni 350 kwa ajili ya ujenzi huo.
Alisema Chuo cha CBE Kampasi ya Mbeya, kilianza mwaka 2013 na wanafunzi 44 na sasa kina wanafunzi 947, ongezeko hilo linaonyesha kuwa, chuo hicho kinaendelea kuaminika zaidi katika utoaji wa elimu ya biashara na ujasiriamali nchini.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Majaliwa amefungua kiwanda cha Raphael Group cha kuongeza thamani zao la mpunga na mengine kilichopo katika eneo la Uyole jijini Mbeya na kumpongeza mwekezaji huyo kwa hatua hiyo.
“Nampongeza Mkurugenzi wa Kiwanda, Raphael Ndelwa, kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Samia za kuhamasisha uwekezaji sambamba na ujenzi wa viwanda ili kuwezesha bidhaa mbalimbali kuzalishwa nchini,” aliongeza.
Aidha, Waziri Mkuu alitoa wito kwa taasisi za serikali zinazojihusisha na sekta ya uwekezaji, kutowasumbua wawekezaji, wawaelimishe na kuwasaidia ili waweze kukuza zaidi shughuli zao.
“Wawekezaji hawa wanaweka pesa nyingi sana katika eneo hilo, ni lazima tuwaunge mkono.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Ndelwa alisema kwamba, kampuni inafanya kazi kwa mfumo wa kilimo cha mkataba na wakulima zaidi ya 14,000 ambao kati yao, 7,800 wamejiajiri katika kilimo cha mpunga na 5,800 wanalima maharage.
NA MWANDISHI MAALUMU