WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Tanzania itaendelea kuunga mkono na kuimarisha ushirikiano uliopo na Umoja wa Afrika, hasa katika kuzingatia misingi ya haki za binadamu na utawala bora, demokrasia na utawala wa sheria.
Amesema hayo, alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, katika ufunguzi wa mkutano wa 64 wa Mwaka wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ambao ulifanyika jijini Arusha.
Majaliwa amesema Serikali ipo tayari kuwapokea na kushirikiana nao pale watakapohitaji ushauri wa aina yoyote. Mkutano huo ulifunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Shirikisho (Majimbo) ya Nigeria, Profesa Yemi Osibanjo.
Amesema mahakama hiyo ilianzishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kwa lengo la kusimamia haki za binadamu, ambapo kwa niaba ya Rais Samia alipata fursa ya kueleza dhamira ya Tanzania katika kuunga mkono jitihada za mahakama hiyo kufanya kazi.
Naye Profesa Osibanjo akizungumzia kuhusu ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika inayolenga kulifanya Bara la Afrika kuwa lenye nguvu duniani katika siku zijazo, alisema ipo haja ya kutambua changamoto zinazokabili Bara la Afrika ili waifikie Afrika wanayoitaka.
Alisema ni muhimu kuangalia namna ya kutafsiri yote yaliyoanishwa katika agenda 2063. “Lazima tutumie fursa na taasisi zote tulizonazo ili tufikie Afrika tunayoitaka lengo ni kuhakikisha tunaona maisha ya Waafrika yanaboreshwa na uchumi unakua,”alisema.
Kwa upande wake, Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud, alitumia fursa hiyo kuishukuru Tanzania kwa ushirikiano wanaoupata ambao unawawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Na Mwandishi Maalumu