MWENYEKITI wa UWT Mkoa wa Dodoma, Neema Majule ameshiriki katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wanawake, Duniani, katika kata ya Msalato, ambayo ni ya kwanza kimkoa kufanya maadhimisho ya siku hiyo.
Mwenyekiti huyo amewapongeza viongozi wa wanawake kata ya Msalato, kwa sherehe hizo na miradi inayofanyika katika kata hiyo pia, kuweza kuunda vikundi 80 vya kinamama.
Neema amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo iliachwa na mtangulizi wake Hayati Dk. John Magufuli.
“Hakika Mama anaupiga mwingi,” Amesema Neema.
Amewatia moyo kina mama kwa kuanisha kazi za maendeleo alizozifanya; kama vile mradi wa shule ya watoto, nyumba ya Katibu wa UWT Mkoa, Fremu za biashara vyumba 10 na mategemeo ya kuanzisha miradi ya kujitegemea kiuchumi, kila wilaya na ameanza utekelezaji wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa UWT kila wilaya.
Aidha, amewasisitiza viongozi wa Kata ya Msalato kufatilia viwanja viwili walivyoahidiwa na Diwani wa kata hiyo pamoja na kibanda cha biashara katika vibanda vilivyopo mnadani pia amewakumbusha viongozi wa kata kuendelea na usajili kwa wanachama na kuhamasisha wanachama ili wajisajili kwa wingi katika mfumo huku akisema ada ya usajili ni rafiki kwa wanachama wote.
Na Mwandishi Wetu