WAZIRI wa Nishati, January Makamba, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kutojiingiza katika siasa, badala yake ametaka mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan yalete tija iliyokusudiwa.
Amesema moja ya mambo anayotaka yashughulikiwe ni kukomesha kukatikakatika kwa umeme ambayo ni changamoto kwa ustawi wa uchumi na kunasababisha manung’uniko kwa wananchi.
Waziri Makamba aliyasema hayo, Jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na watendaji wakuu wa shirika hilo, ikiwemo bodi mpya ya wakurugenzi, menejimenti na wakuu wa kanda wa shirika hilo.
“Agizo langu ni hili naomba kila mmoja anapotekeleza majukumu yake ahakikishe anazingatia na sitaki kusikia katikakatika ya umeme, ikomeshwe mara moja. Rais Samia Suluhu Hassan ametuamini, hivyo tuchape kazi, tuondoe maneno na manung’uniko ya wananchi,” alisema.
Waziri Makamba alisema lengo la Rais Samia kufanya uteuzi na utenguzi katika shirika hilo anataka kuona mapinduzi makubwa ndani ya shirika hilo.
“Inawezekana Rais ameona mbali maana alivyoniteua kuwa Waziri wa Nishati amenipa maagizo nianze na TANESCO hata kwa kuifumua upya ili kuleta mabadiliko yanayostaili”alisema
Amesema kilichokuwa kinasababisha shirika kusuasua ni utendaji na uendeshaji usioleta tija, lakini uteuzi uliofanywa na Rais anaamini utaleta mafanikio.
“Tunaanza safari mpya ya kuiendesha TANESCO, kwa sababu ni shirika la kimkakati, hivyo ni lazima lifanye kazi zake kibiashara ili liweze kulipatia faida Taifa,” alifafanua.
Alisema licha ya serikali kutaka kuondoa changamoto ya kukatika kwa umeme, kila wakati pia inataka kuona shirika hilo linauza umeme wake katika nchi za jirani.
“Shirika lina uwezo mkubwa wa kuuza umeme katika nchi zinazotuzunguka kinachotakiwa ni ufanisi na ubunifu kwa kuwa tayari tuna vyanzo vingi vya kupatikana kwa umeme,”alisema.
Aidha alisema hataki kuona shirika linaendeshwa kimazoea ila linatakiwa liendeshwe kimkakati ili liongeze ti ja zaidi.
Katika mkutano huo Waziri Makamba alisema katika mabadiliko anayoanza nayo sasa, hata siku moja hatokubali kumvumilia mtendaji ambaye ni mbadhirifu, mdanganyifu na mwizi ndani ya shirika .
Waziri Makamba alisema, hakuna kitu kigumu kama kumtoa mtu katika madaraka yake, lakini wakati mwingine inabidi ifanywe hivyo ili mambo yaende sawa.
Vilevile aliwambia viongozi hao kwamba mabadiliko hayo waliyoyapokea wayatekeleze inavyostaili na hategemei kuwa yatazaa migogoro na minon’gono ya chini chini.
Naye, Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato, alisema anategemea mambo makubwa kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia.
“Fanyeni vizuri watendaji wetu ili mimi nikiwa pale Bungeni naulizwa maswali niweze kujibu kwa ufasaha na kujiamini zaidi”alisema
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Chande Maharage, alisema kikubwa atakachoangalia ni kuwaondolea wateja changamoto zinazowakabili zikiwemo za kukatika kwa umeme.
“Baada ya kikao hiki nitakaa pamoja na menejimenti yangu ili tujadiliane jinsi ya kutatua matatizo yaliyopo ndani ya shirika, hasa kwa wateja wetu,” alisema Maharage.
Maharage alisema anataka kuondoa changamoto za rasilimali watu na yule anayefanya vizuri atatakiwa kupewa stahiki yake ili kuongeza ufanisi zaidi katika shughuli zao.
“Hatuwezi kuwa na mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme na majengo makubwa, huku hali za wafanyakazi hadhiridhishi,” alisema Maharage
Mwenyekiti mpya wa bodi hiyo, Omari Issa, alisema watafanya kila linalowezekana ili kufikia malengo mazuri na yanayokubalika na Taifa katika suala zima la umeme.
“Nahakikisha hatutawaangusha tutafanya vile inavyotakiwa, lakini kila mmoja wetu anatakiwa kubadilika na akubali mabadiliko yaliyopo,” alisema.
Na REHEMA MAIGALA