SERIKALI imesema mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme wa megawati 2,115 wa Julius Nyerere unatarajiwa kukamilika bila ongezeko la gharama za ujenzi.
Waziri wa Nishati, January Makamba, aliyasema hayo alipotembelea eneo la mradi akiambatana na Waziri wa Nyumba Maendeleo ya Makazi na Huduma wa Misri, Assem Hafez El azar.
Ziara hiyo ilikuwa ya pamoja kati ya Tanzania na Misri, ambapo wamepokea taarifa ya utekelezaji wa mradi ya Novemba, mwaka huu, inayoonyesha kuwa, utekelezaji wa mradi unakwenda vizuri.
“Kwa dhamira na malengo ya mradi na gharama zilizotumika, serikali ya Tanzania haiwezi kuruhusu mradi huu kutokukamilika, kwa wenzetu wa Misri pia mradi huu ni chachu ya ushirika yenye manufaa kwao, nao pia wako tayari kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa faida ya nchi zote mbili,” alisema.
Aliielekeza timu ya wataalamu ya Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuangalia changamoto zilizojitokeza na kuzifanyia kazi ili kuhakikisha mradi unakamilika kama Rais Samia Suluhu Hassan alivyowaahidi Watanzania.
Mhandisi El azar ambaye ni Waziri wa Nyumba, Maendeleo ya Makazi na Huduma wa Misri, alisema serikali ya nchi yake inawahakikishia Watanzania kuwa, mradi wa JNHPP ni muhimu kwa nchi zote mbili ili kujenga uhusiano na imani kwa Watanzania kuwa Misri ni nchi nyenye uwezo wa kutekeleza miradi mingine mikubwa ambayo Tanzania itatazamia kuitekeleza.
Katika ziara hiyo, Makamba aliongozana na Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Maharage Chande na wataalamu mbalimbali wa Wizara ya Nishati ambao wamekagua pia maeneo muhimu ya mradi yanayoendelea kujengwa ambayo ni nyumba ya mitambo, sehemu ya kupokea umeme na eneo linapojengwa daraja.
Kukamilika kwa wakati kwa mradi wa Julius Nyerere, kutasaidia nchi kupata umeme wa uhakika, bora na wa gharama nafuu, hivyo kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wataalamu mbalimbali.
Na MWANDISHI WETU