WAZIRI wa Nishati, January Makamba, ameeleza kuwa wakuu wa mikoa minane ambayo itapitiwa na bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), wanajukumu la kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unafanikiwa.
Amewataka kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuhakikisha fursa zitakazopatikana zinanufaisha wananchi wa mikoa yao.
Makamba aliyasema hayo wakati wa semina kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa itakayopitiwa na mradi huo, inayoendelea jijini Tanga.
“Moja ya sababu za bomba hili kupita nchini kwetu ni uhakika wa ulinzi na usalama uliopo. Usalama huo utaendelea kuwepo kama wanaosimamia usalama huo kwenye maeneo linapopita bomba wana uelewa kuhusu mradi na kile kinachohitajika kufanywa, ili walioamua bomba hili lipitie kwetu wawe na imani kwamba walifanya uamuzi sahihi,” alisema Makamba.
Aliongeza kuwa semina hiyo inalenga kutengeneza uwelewa mpana kwa viongozi hao kuhusu mradi na kujadili fursa mbalimbali zitakazopatikana katika utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato alitoa rai kwa viongozi hao kuhakikisha wanatengeneza mazingira mazuri, ili fursa zitakazotokana na utekelezaji wa mradi huo zinufaishe wananchi wa mikoa husika.
Byabato alisema kuwa bomba hilo litapita katika mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.
Alieleza kuwa, mkataba hodhi wa mradi baina ya serikali na kampuni ya bomba, umeainisha baadhi ya bidhaa na huduma zitakazotolewe na Watanzania pekee.

Naibu Waziri Byabato aliongeza kuwa bidhaa na huduma hizo ni pamoja na usafirishaji, ulinzi, chakula na vinywaji, huduma ya malazi, mafuta kwa ajili ya magari na mitambo, shajala, bidhaa za ujenzi zinazopatikana nchini, shughuli za ujenzi, huduma za mawasiliano na ukodishaji wa mitambo ya ujenzi.
Byabato alisema bidhaa na huduma nyingine za ununuzi tofauti na zile zilizotengwa kwa Watanzania, zitapatikana kwa njia ya ushindani na Watanzania wenye uwezo, vigezo na sifa stahiki wataruhusiwa kushiriki.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Dk. James Mataragio, alieleza kuwa serikali kupitia shirika hilo inamiliki asilimia 15 ya hisa katika utekelezwaji wa mradi huo, huku asilimia 62 zikishikiliwa na Kampuni ya Total Energies, asilimia 15 ni za UNOC ya nchini Uganda, huku CNOOC ikishikilia asilimia 8.
“Majukumu ya TPDC kwenye mradi huu ni pamoja na kuwa mbia kwenye mradi wenyewe, kushughulikia masuala ya ardhi, kusimamia mikataba yote ya EACOP, kuwa na uwakilishi wa asilimia 15 kwenye uongozi na kuwa na mjumbe kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya EACOP, pamoja na kuratibu ushirikishwaji wa wadau mbalimbali watakaofanikisha utekelezaji wa mradi huu,” aliongeza.
Semina hiyo iliwakutanisha wakuu wa mikoa hiyo jijini Tanga, pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali, bunge, Wizara ya Nishati na taasisi zake, itafanyika kwa siku tatu na itamalizika leo.
Na MWANDISHI WETU