KAMISAA wa Sensa ambaye pia ni Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda, amewataka vijana kutoka vyuo vikuu, kutumia mitandao ya kijamii kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi.
Makinda ametoa rai hiyo Jijini Dodoma, wakati wa kongamano la umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi, lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHILISO).
Amesema sensa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kwa kuwa inasaidia taifa kupata takwimu sahihi ya watu wake ili kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.
“Wanafunzi wa vyuo vikuu ni mafundi wa kutumia mitandao, tumieni kuwaelimisha wananchi umuhimu wa sensa na kuhamasisha kuona umuhimu wa kushiriki shughuli hiyo wakati utakapofika
“Kila unapoingia katika mtandao hakikisha unaweka ujumbe unaohusu sensa, utakuwa umefanya suala la kizalendo kwa taifa lako,” alisema.
Kuhusu suala la usiri, alisema makarani kabla ya kuanza kazi ya kukusanya taarifa wataapishwa kiapo cha kutunza siri na ikitokea akatoa siri atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kiapo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Keneth Hosea, amesema wanaunga mkono sense na aliitaka TAHILISO kuwa mabalozi wa kutangaza na kutoa elimu kwa umma.
Na Happiness Mtweve, Dodoma