Na HAWA NGADALA
MKAZI wa Mabibo farasi, Alafa Mwalimu, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kwa shitaka la kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi gramu 21.25 .
Alafa (30), alifikishwa mahakamani hapo juzi na kusomewa shitaka hilo na wakili wa serikali, Debora Mushi, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Aaron Lyamuya.
Debora alidai mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo, Februari mosi, mwaka huu, eneo la Mabibo farasi, Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, kwa kukutwa akimiliki kiasi kidogo cha dawa za kulevya aina ya bangi.
Mshitakiwa alikiri kutenda kosa hilo ambapo upande wa jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
Pia, upande wa Jamuhuri uliiomba mahakama kupanga tarehe na kuiandika barua kituo cha polisi cha Mburahati kwa ajili ya kuleta vithibiti hivyo.
Mshitakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kuiomba mahakama kujidhamini kutokana na hali ya maisha aliyonayo.
“Mheshimiwa hakimu naomba kujidhamini mwenyewe kutokana na hali ya maisha niliyonayo, mimi ni mama mwenye watoto sita ambao hawana baba.
Ni kweli nimekamatwa nayo na ilikuwa siku yangu ya kwanza kufanya biashara hiyo na watoto wote wananitegemea, endapo nikirudi mahabusu hao walioko nyumbani wataathirika katika jamii,” alidai mshitakiwa huyo.
Hakimu alimweleza mshitakiwa kuwa dhamana yake iko wazi atadhaminiwa kwa barua ya polisi na kumtaka kuripoti kila baada ya wiki katika kituo cha polisi cha Mburahati chini ya polisi mpelelezi wa shauri hilo.
Mshitakiwa yupo nje kwa dhamana hiyo na shauri liliahirishwa hadi Aprili 13, mwaka huu.