MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), imesema suala la mabasi ya abiria maarufu kama daladala kubeba abiria kulingana na idadi ya viti ‘level seat’ ili kuepusha maambukizi ya ugonjwa ni changamoto kutokana na idadi kubwa ya wasafiri na mabasi kutokidhi mahitaji.
Kutokana na hali hiyo, LATRA imeiomba serikali kutoa vibali vya muda kwa magari binafsi ili yaruhusiwe kubeba abiria kuepusha msongamano ndani ya mabasi ya daladala.
Akizungumza na Uhuru Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Utumiaji wa Usafiri wa Ardhi (LATRA CCC), Leo Ngowi, alisema kuna umuhimu wa kuongeza magari ya abiria ili wasafiri wapate huduma hiyo kwa urahisi katika kipindi hiki cha kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Pia, Ngowi aliiomba serikali kutoa fursa kwa magari hususan ambayo hayajasajiliwa, kubeba abiria, lakini yapewe vibali vya muda kwa ajili ya kutoa huduma hiyo.
Hiyo ni moja ya hatua za kupunguza msongamano katika mabasi yanayotoa huduma hiyo kwa sasa.
“Ili kupambana na uviko – 19, ni vyema kufuata mwongozo wa wizara husika (Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) ili kuepukana na maambukizi yanayoweza kutokea katika mkusanyiko wa watu,” alisema Ngowi.
Ngowi alisema katika mlipuko wa kwanza wa uviko -19, serikali ilitoa usajili mfupi wa magari 400 kwa ajili ya kubeba abiria majira ya asubuhi na jioni.
Aliliomba Jeshi la Polisi, kusimamia kwa karibu mwongozo unaotaka magari kuepuka kusimamisha abiria kupita kiasi hasa baada ya vibali kutolewa na magari kuongezeka.
“Jeshi la polisi kuweni makini na daladala ambazo zitaonyesha utovu wa nidhamu wa kusimamisha abiria wakati serikali ikiwa imeongeza magari ya ziada,” alisema.
Hata hivyo, Ngowi alisema serikali katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa huo, kutazamwe njia mbalimbali zitakazoepusha msongamano.
Akitolea mfano, alisema inaweza kuamua maduka yaanze kufunguliwa kuanzia saa 4.00 asubuhi huku ofisi zingine zipange muda tofauti wa kuanza kazi, lengo ni kutoa fursa kwa wasafiri kupanda vyombo vya usafiri vya umma katika muda tofauti.
“Zipo baadhi ya nchi zilishawahi kupeana nafasi ya kufanya shughuli za kila siku ili kuepusha msongamano ambao ni hatari kwa kusambaa virusi vya corona.”
Kwa upande wa abiria, aliwataka waheshimu miongozo na utaratibu uliotangazwa na serikali kwa ajili ya kujikinga dhidi ya uviko 19.
Na REHEMA MAIGALA