SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na serikali ya Marekani, wameleta chanjo milioni moja kwa ajili ya kuwachanja wananchi kama hatua ya kuzuia maambukizi makali na mapya ya ugonjwa wa corona.
Mkuu wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID), Kate Somvongsir, amesema hayo katika mkutano wa pamoja wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa kupata habari, yaliyoandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la ‘Internews,’ uliofanyika kwa njia ya mtandao na kushirikisha waandishi wa habari.
“Marekani na Tanzania tuna ushirikiano wa miaka 60 sasa, katika masuala mbalimbali ya kuleta maendeleo ya watu wetu, ikiwemo kuhakikisha wanaendelea kuwa na afya bora, ndiyo maana Marekani imeamua kutoa chanjo milioni moja inayotengenezwa na Kampuni ya Johnson & Johnson,” alisema.
Kate aliongeza kuwa, hiyo ni kwa ajili ya kuwakinga wananchi wa Tanzania.
“Tunaomba wananchi wajitokeze na kuchangamkia chanjo hiyo kwani ni salama,” alieleza Kate.
Kwa upande wake, Ofisa Habari kutoka Mahakama Kuu, Faustine Kapama, aliwashauri waandishi wanaoandika habari za mahakamani, kufahamu sheria na vifungu vinavyowalinda na vinavyowazuia kuandika baadhi ya habari mfano, zinazohusu watoto wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Naye Patrick Kipangula, kutoka Idara ya Habari (MAELEZO), aliwakumbusha waandishi wa habari ambao bado hawajafikia takwa la sheria la vyombo vya habari kuwa na elimu ngazi ya diploma, kufanya hivyo, wasibweteke bali waendelee kujisomea.
Na ANGELA SEBASTIAN, Bukoba