WATANZANIA wametakiwa kujitokeza kwa wingi kusajili biashara zao ili kuongeza wigo ya ufanyaji wa biashara ndani na nje ya nchi kisheria.
Kauli hiyo ilitolewa na Ofisa Leseni wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Robert Mashika, katika maonesho ya “Kamilika 2022” yanayoendelea eneo la Mlimani City Dar es Salaam.
Amesema mjasiriamali akisajili biashara yake ataweza kuongeza wigo mkubwa wa ufanyaji wa biashara popote atakapokuwa.
Mashika ametaja faida za kusajili bashara ni mjasiriambali kuweza kufanya biashara kubwa, kuipa utu na nafasi biashara yake.
Ametaja faida nyingine ni mfanyabiashara kuongeza imani na taasisi za fedha zinazokopesha, kupata tenda kubwa.
Nyingine ni kukuza uwekezaji na mataifa mengine na mfanyabiashara kuweza kulinda jina la bishara yake ili lisiweze kuchukuliwa na mtu mwingine.
Ofisa huyo amesema katika maonesho yanayofanyika Mlimani City, BRELA imewahudumia watu zaidi ya 1000.
Aidha, amesema wakala huo umeweka mikakati ya kuwafuata wateja katika miji yote mikubwa ya kibiashara ambapo kwa mwaka huu wameanza na Dar es Salaam.
Amebainisha kuwa zoezi hilo litakuwa ni endelevu na wameamua kulifanya baada ya kupokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi yakiwa ya kutojua matumizi ya teknoloji wakati wa usajili.
Hata hivyo maonesho hayo yamekuwa yakitoa elimu kwa umma lengo likiwa ni kuwafikia wadau wakuu ndio maana wanakaa eneo lenye mwingiliano mkubwa wa watu.
Na ATHNATH MKIRAMWENI