TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi imewaonya na kuahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria matapeli wote wanaojifanya maofisa wa taasisi hiyo wanaochafua taswira na imani ya chombo hicho cha serikali kwa wananchi.
Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Katavi,Fautine Maijo ameyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu kwa waadishi wa habari ofisi kwake.
Licha ya kuelezea mafanikio makubwa waliyoyapata, pia aliwaonya vikali watu wenye nia mbaya ya kuharibu taswira ya taasisi hiyo.
Maijo amesema kuwa kumekuwa na wimbi la matapeli wanaojitambulisha kama wao ni maofisa wa Takukuru na hupiga simu kwa watu mbalimbali wakitoa maelekezo ya maagizo kwa watu hao, ikiwa ni pamoja na kutakiwa kuripoti ofisi fulani ya Takukuru.
“ Wanahabari, matapeli hao hutaka kuonana na wahusika na wamekuwa wakiwatapeli wananchi na baadhi ya watumishi kwa namna nyingi,” amesisitiza Maijo.
Kaimu wa Takukuru huyo licha ya kukemea vikali tabia hiyo na kuwataka waache mara moja aidha aliwaambia wananchi kutambua haki yao ya kuhoji utambulisho wa mtu yeyote anayejitambulisha kuwa ni ofisa wa Takukuru.
Aidha, amewaeleza mwananchi kuwa, yeyote anayepewa wito wa kuitwa na maifisa wa Takukuru wanapaswa kujiridhisha kwa uhakika kuwa unakokwenda ni ofisi kweli za Takukuru na si kwingineko na endapo utapata mashaka jiridhishe na ofisi ya takukuru iliyo karibu sambamba na kupiga simu ya dharura 113 bure.
Vilevile alitoa wito kwa wananchi wote kutokubali kutapeliwa na kupaswa kutoa taarifa Takukuru ili mhalifu huyo achukuliwe hatua za kisheria, kwani ni kosa la kisheria kujifanya ofisa wa Takukuru.
Katika hatua nyingine, takukuru mkoa wa Katavi kwa kipindi cha Aprili hadi Juni,2021 imefanya kazi ya ufuatiliaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo mitatu yenye jumla ya sh. 1,756,702,580 na kubaini kuwepo kwa upungufu wa kiutendaji.
Na George Mwigulu,Katavi.