POLISI Mkoa wa Katavi, imekamata dawa za kulevya aina ya bangi, gongo na gobore katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ali Makame Hamad, aliyasema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Alisema walimkamata Anastazia Joseph (47), mkazi wa Mtaa wa Society, akiwa na kete 432 na gramu 1,250 za bangi.
Hamad aliongeza kuwa katika kipindi cha wiki moja kuanzia Desemba 18 hadi Desemba 24, mwaka huu, waliwatia mbaroni watuhumiwa 13, baada ya kukamatwa na lita 317 za gongo.
Pia alisema wanamshikilia William Chacha (20), mkazi wa Kitunda kwa tuhuma za kukutwa na goboRe katika kijiji cha Wachawaseme, Kata ya Utende, Tarafa ya Inyonga, Wilaya ya Mlele.
Kamanda huyo alisema silaha hiyo ilisalimishwa katika ofisi ya mtendaji wa kijiji hicho na watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Katika hatua nyingine, kamanda huyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanachukua tahadhari kipindi hiki cha sikukuu katika kukabiliana na changamoto za matukio ya uhalifu.
“Wananchi wanapaswa kuepuka mazingira hatarishi wakati wa sikukuu kwa kutosherehekea mbali na makazi ya watu na ulevi wa kupita kiasi”.
Kuhusu madereva, aliwataka kufanyia matengenezo vyombo vyao na kuzingatia sheria za usalama barabarani na wazazi, walezi kulinda usalama wa watoto.
Kamanda Hamad alisema jeshi hilo limejipanga kudumisha hali ya ulinzi na usalama kwa kufanya doria usiku na mchana katika maeneo yote.
Na George Mwigulu, Katavi